WATU WATANO WAFARIKI KWA KUFUKIWA NA KIFUSI MGODINI GAIRO
Na Joseph Ngilisho-#ArushaDigitalUpdate #| MOROGORO
WATU watano wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi wakiwa ndani ya duara la mgodi wa Kitaita, Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, walikokuwa wameingia kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhar Kubecha, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema marehemu hao, ambao hutambulika kwa jina la “wadudu”, walikuwa miongoni mwa watu tisa walioingia kinyemela mgodini nyakati za usiku kufanya uchimbaji bila idhini.
Kubecha amesema kifusi kilianguka ghafla na kuwafukia, hali iliyosababisha vifo vya watu hao watano.
Amesema hadi sasa mwili wa mtu mmoja pekee ndiyo umefanikiwa kutambuliwa, huku miili mingine minne ikiwa bado haijafahamika majina kutokana na taarifa kwamba wengi wa waathirika walitoka nje ya Wilaya ya Gairo.
Mamlaka za wilaya zinaendelea na taratibu za uokoaji, uchunguzi na utambuzi wa miili hiyo, huku viongozi wakitoa wito kwa wachimbaji kuacha kuingia migodini kinyemela, hususan nyakati za usiku, kutokana na hatari ya kupoteza maisha.
Tukio hilo limeongeza wito kwa mamlaka na wachimbaji kuimarisha usalama katika maeneo ya migodi ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.
NB:Picha ni Kwa hisani ya Mtandao
Ends

إرسال تعليق