VISION FUND YAFUNGUA NJIA MPYA YA MIKOPO, YAONDOA MAKATO YA MIAMALA
...YAZINDUA SMART BANKING; WANANCHI KUFUNGUA AKAUNTI, KUWEKA AKIBA NA KUKOPA KIDIGITALI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
TAASISI ya Fedha ya VISION Fund Tanzania Microfinance Bank imezindua mfumo mpya wa kidigitali wa VFT Smart Banking, unaowawezesha wananchi kufungua akaunti, kuweka akiba, kufanya miamala na kupata mikopo bila dhamana kwa kuzingatia nidhamu yao ya kuweka akiba.
Mfumo huo pia umeondoa makato kwenye miamala mbalimbali inayofanyika kupitia huduma hiyo, hatua ambayo uongozi wa Vision Fund unasema inalenga kupunguza gharama zinazowakabili wananchi na kuchochea matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa njia ya kidigitali.
Uzinduzi huo umeboresha matumizi ya teknolojia kama njia ya kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini na yaliyo mbali na matawi ya taasisi za kifedha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo, Septemba 01,2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Vision Fund Tanzania Microfinance Bank, Rogate Godson Mwangi, alisema VFT Smart Banking imebuniwa kukabiliana na changamoto kuu zinazowakabili wananchi katika kupata huduma za kifedha, ikiwamo gharama za miamala, umbali wa kufikia huduma na ugumu wa kupata mikopo kwa watu wasiokuwa na dhamana.
“VFT Smart Banking inakuja kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali ambazo tumezibainisha katika huduma za kifedha, ikiwemo gharama za kufanya miamala, upatikanaji wa mikopo bila dhamana, pamoja na changamoto ya umbali,” alisema Mwangi.
Alisema teknolojia hiyo inampa mwananchi uwezo wa kupata huduma za kifedha akiwa eneo alilopo bila kulazimika kusafiri kwenda katika tawi la benki.
Mwangi alisema moja ya mambo makubwa yaliyowekwa kwenye mfumo huo ni kuondoa gharama za miamala, akieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubaini kuwa makato yamekuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowafanya wananchi kusita kutumia huduma za kifedha kidigitali.
Alisema wananchi sasa wanaweza kutumia mfumo huo kufanya malipo mbalimbali, ikiwamo kulipia bili, huduma na kuhamisha fedha, bila kubebeshwa gharama za miamala kupitia mfumo huo.
“Watu wengi wamekuwa wakilalamikia gharama za makato wanapofanya malipo ya bili, kulipa tozo mbalimbali au kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine. Kwa kuona changamoto hiyo, sisi tumeondoa hizo gharama,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwangi, uamuzi huo unalenga kuwafanya wananchi wengi zaidi waone matumizi ya huduma za kidigitali kuwa rahisi na yenye gharama nafuu.
Katika eneo la mikopo, Vision Fund imeweka mfumo unaompa mteja nafasi ya kujenga historia yake ya kifedha kupitia nidhamu ya kuweka akiba, ambayo inaweza kutumika katika tathmini ya uwezo wake wa kupata mkopo bila dhamana.
Mwangi alisema mfumo huo ni muhimu kwa wananchi wenye uwezo wa kurejesha mikopo lakini ambao wamekuwa wakikosa fursa hiyo kutokana na kutokuwa na dhamana zinazohitajika na baadhi ya taasisi za kifedha.
“Ni application ambayo itawasaidia watu waweze kukopa vile watakavyoweza kuonyesha nidhamu yao ya kuweka akiba. Wanaweza kukopa bila kuwa na dhamana,” alisema.
Hatua hiyo inaifanya akiba kuwa siyo tu njia ya kutunza fedha, bali pia kuwa sehemu ya kujenga uaminifu wa kifedha wa mteja.
Mkurugenzi wa Fedha wa Vision Fund Tanzania, Henry Horombe, alisema taasisi hiyo ambayo imekuwa ikitoa huduma za kifedha kwa zaidi ya miaka 30, inalenga zaidi wananchi wa kawaida, wajasiriamali na makundi mbalimbali yanayokidhi vigezo vya kupata huduma hizo.
Horombe alisema matumizi ya teknolojia yamefungua fursa mpya ya kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja, badala ya kutegemea uwepo wa matawi pekee.
“Kwa kutumia digitali ama teknolojia, tunaweza kufikia watu wengi zaidi na kuwawezesha kupata au ku-access huduma za mikopo,” alisema.
Alisema kupitia VFT Smart Banking, mteja anaweza kufungua akaunti, kuweka akiba na kupata huduma za mikopo, huku mfumo ukiwawezesha pia kufanya malipo mbalimbali bila gharama za miamala.
Horombe alisema Vision Fund pia inaendelea kutoa huduma ya Dunduliza, inayolenga kuwawezesha wanachama wa vikundi kuweka akiba kwa pamoja na baadaye kupata fursa ya huduma za mikopo.
Alisema falsafa ya huduma hizo ni kumwezesha mwananchi kuanza na kiasi kidogo, kujenga utamaduni wa kuweka akiba na hatimaye kutumia historia hiyo katika kupata huduma nyingine za kifedha.
“Si lazima unapokuwa unafanya miamala au unapotumia huduma za kifedha uwe na pesa nyingi. Mfumo huu unamwezesha mwananchi wa kawaida kuanza kidogo kidogo,” alisema.
Horombe alisema mikopo yenye masharti rafiki inaweza kuwa kichocheo cha ukuaji wa shughuli ndogo za kiuchumi na kuongeza kipato cha familia.
Alisema mzazi anapopata mtaji na kuanzisha au kukuza shughuli ya kiuchumi, matokeo yake yanaweza kuonekana moja kwa moja katika maisha ya familia, ikiwamo uwezo wa kugharamia elimu na mahitaji mengine muhimu ya watoto.
“Mzazi akipata pesa, akapata mkopo na kuingia kwenye mfumo wa kibenki, kukawa na shughuli za kiuchumi zinazoongeza kipato cha familia, basi tunakuwa na athari chanya kwa familia nzima,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Vision Fund Tanzania, Deogratias John Siria, alisema mfumo huo umejengwa katika misingi mitatu mikuu; kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuwajengea wateja uwezo wa kupata mikopo kupitia akiba na kuwapa huduma za kibenki bila kujali walipo.
Alisema mwananchi anaweza kufungua akaunti kwa kutumia simu yake na kufanya miamala bila kulazimika kufika katika tawi la benki.
“Mtanzania yeyote atakuwa na uwezo wa kufungua account sehemu yoyote alipo, atakuwa na uwezo wa kufanya transactions za kibenki sehemu yoyote alipo bila kushindwa kufika kwenye tawi la benki,” alisema.
Siria alisema pamoja na kurahisisha huduma, Vision Fund imeweka mkazo mkubwa katika usalama wa taarifa na fedha za wateja wanaotumia mfumo huo.
Alisema hatua mbalimbali za kiusalama zimewekwa katika mfumo huo ili kuzuia watu wasiohusika kuingia kwenye akaunti za wateja au kuiba taarifa zao.
“Vision Fund Smart Banking imezingatia mambo yote ya usalama. Kwa hiyo mteja anapofungua account kwa kutumia njia ya kidijitali, kuna taratibu za usalama ambazo zimewekwa za kuweza kuzuia wizi wa passwords,” alisema.
Alisema mfumo huo ulifanyiwa User Acceptance Testing (UAT) kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa umma, hatua iliyolenga kuhakikisha huduma hiyo inafanya kazi kwa ufanisi na kwa usalama.
Mwangi alisema kuongezeka kwa matumizi ya simu janja nchini ni fursa muhimu kwa taasisi za kifedha kuwafikia wananchi ambao awali walikuwa na changamoto ya umbali au gharama za kufuata huduma.
Alisema Vision Fund inalenga kutumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi zaidi kujiunga na huduma za kifedha kidigitali.
“Tunafahamu kwamba Watanzania wengi zaidi sasa wanatumia smartphone. Kwa sababu hiyo, tumeamua kuleta mageuzi katika matumizi ya smartphone na kuleta application ambayo ni nafuu sana kwa wateja wetu,” alisema.
Uzinduzi wa VFT Smart Banking unaifanya Vision Fund Tanzania kuingia katika hatua mpya ya matumizi ya teknolojia katika huduma za kifedha, huku akiba, mikopo, miamala na usalama vikiunganishwa kwenye mfumo mmoja unaolenga kumfikia mwananchi bila kujali eneo alipo.
Kwa mtazamo wa Vision Fund, teknolojia siyo tena njia ya kuongeza kasi ya huduma pekee, bali imekuwa daraja la kumfikishia mwananchi wa kawaida huduma za kifedha, mtaji na fursa za kukuza kipato.
Ends








Post a Comment