Breaking🔥

UGOMVI WA KUGOMBEA MAENEO YA MAJI WAIBUKA NGORONGORO, WAMASAI NA WADATOGA WAZICHAPA VIJANA WAWILI WA KIMASAI WAUAWA, MAKALLA AAGIZA WAHUSIKA WAKAMATWE

VIJANA WAWILI WA KIMASAI WAUAWA, MAKALLA AAGIZA WAHUSIKA WAKAMATWE

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


VIJANA wawili kutoka jamii ya Kimasai wameuawa katika mgogoro wa kugombea maeneo yenye vyanzo vya maji kati ya jamii za Kimasai na Wadatoga katika Kata za Kakesio na Eyasi, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika na mauaji hayo.

Makalla alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi wa jamii hizo mbili katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kakesio.

Mkutano huo ni sehemu ya jitihada za kutafuta suluhu ya mgogoro huo ambao umehusishwa na ushindani wa maeneo yenye vyanzo vya maji ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Alikemea vikali mauaji hayo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza kuwa migogoro inapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na kupitia mamlaka zinazohusika.

“Nawaagiza Polisi wawatafute, wawakamate na kuwachukulia hatua wote waliohusika na mauaji haya. Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi,” alisema Makalla.

Katika hatua nyingine, Makalla ametangaza kuunda timu ya wataalamu itakayojumuisha vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini chanzo cha migogoro hiyo.

Timu hiyo pia itachunguza madai ya kuwepo kwa baadhi ya wananchi kutoka mikoa ya jirani wanaodaiwa kuvamia maeneo ya hifadhi, hali inayodaiwa kuchochea migogoro ya ardhi, maji na malisho.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Jeshi la Polisi limeanza kuwatafuta na kuwakamata wote wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Naye Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, amezitaka jamii za Kimasai na Wadatoga kudumisha amani na utulivu, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro inayohusu visima, vyanzo vya maji na maeneo ya malisho.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم