Breaking🔥

TANZANIA, ALGERIA ZAFUNGUA NJIA MPYA YA USHIRIKIANO VIWANDA VYA DAWA

TANZANIA, ALGERIA ZAFUNGUA NJIA MPYA YA USHIRIKIANO VIWANDA VYA DAWA

Na Joseph Ngilisho |Arushadigital

TANZANIA imeanza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Algeria katika sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo nchini na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.

Hatua hiyo imekuja baada ya Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda vya Dawa wa Algeria, Dkt. Wassim Kouidri, katika ofisi za wizara hiyo jijini Algiers.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Matinyi alimweleza Waziri Kouidri kuhusu mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kukuza sekta ya viwanda vya dawa ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kutumia fursa ya soko kubwa la Afrika, hususan katika ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Alisema Serikali imeweka vivutio maalum kwa wawekezaji katika sekta hiyo na kwamba tayari viwanda vitano vya dawa vinaendelea kujengwa nchini, huku vingine vikitarajiwa kuanzishwa.

“Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya dawa na vifaa vya tiba katika ukanda wa nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika wenye watu takribani milioni 350,” alisema Balozi Matinyi.

Kwa upande wake, Waziri Kouidri aliahidi ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika kuisaidia Tanzania kupata utaalamu na teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

Alisema Tanzania iko katika eneo la kimkakati lenye fursa kubwa ya soko, hivyo Algeria iko tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha inafikia malengo yake ya kukuza sekta hiyo.

“Ni kweli, Tanzania ipo kwenye eneo zuri la kimkakati la ukanda mkubwa wa Afrika na Algeria iko tayari kushirikiana nayo kitaalamu ili kuhakikisha inafikia malengo yake,” alisema Waziri Kouidri.

Katika hatua nyingine, Balozi Matinyi alikaribisha nchini Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP), ambayo inatarajiwa kutembelea Tanzania mwezi Oktoba mwaka huu kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).

Ziara hiyo inatarajiwa kujikita katika kujadili na kuweka mikakati ya ushirikiano wa kitaalamu, ikiwamo masuala ya udhibiti, usalama, ubora na uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

Tanzania tayari ina nafasi muhimu katika mifumo ya udhibiti wa dawa barani Afrika baada ya kuwa nchi ya kwanza barani kufikia Kiwango cha Tatu cha Ukomavu (ML3) mwaka 2018, chini ya tathmini ya Global Benchmarking Tool (GBT) ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

ML3 ni miongoni mwa viwango vinavyotumika kutathmini uwezo na ubora wa mifumo ya kitaifa ya udhibiti wa dawa.

Tangu mwaka 2020, nchi nyingine tisa za Afrika zimefikia kiwango hicho, ambazo ni Afrika Kusini, Ethiopia, Ghana, Misri, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal na Zimbabwe, huku hakuna nchi ya Afrika iliyofikia kiwango cha juu zaidi cha ML4.

Kwa upande wa Algeria, nchi hiyo imejijengea nafasi kubwa katika sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba barani Afrika, ikiwa na takribani viwanda 230, sawa na karibu theluthi moja ya viwanda 690 vya aina hiyo vilivyopo barani Afrika.

Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria unatarajiwa kuongeza fursa za uhamishaji wa teknolojia, utaalamu na uwekezaji katika sekta ya dawa, hatua inayoweza kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuongeza uwezo wa Tanzania kuhudumia soko la Afrika.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم