Breaking🔥

NDONDE ATIWA MBARONI NA POLISI KWA WIZI WA GARI LA CHADEMA KANDA YA KASKAZINI

NDONDE MBARONI KWA TUHUMA ZA WIZI WA GARI LA CHADEMA KANDA YA KASKAZINI 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Ndonde

ALIYEKUWA Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Ndonde Totinan, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, kwa tuhuma zinazohusishwa na wizi wa gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 523 EMK,  mali ya chama hicho.

Ndonde, ambaye kwa mujibu wa viongozi wa CHADEMA alijiondoa katika chama hicho tangu Aprili Mosi, 2026, anashikiliwa na Polisi baada ya gari hilo kukamatwa kwa ushirikiano wa chama hicho na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Yohana Kaunya, amesema gari hilo pamoja na baadhi ya mali nyingine za chama zilikuwa zikishikiliwa na Ndonde baada ya kuondoka katika nafasi yake.

Kaunya amesema chama hicho kilichukua hatua ya kufuatilia mali hizo na kushirikiana na Jeshi la Polisi hadi kufanikisha kupatikana kwa gari hilo na kukamatwa kwa Ndonde aliyekuwa ametokomea na mali hizo .

Amesema kwa sasa CHADEMA inasubiri hatua zaidi za kisheria kutoka kwa Jeshi la Polisi, ambalo bado halijatoa taarifa rasmi kuhusu mashtaka yatakayomkabili Ndonde.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure, amesema kushikiliwa kwa mali hizo, ikiwemo gari hilo, kumeathiri utekelezaji wa shughuli za chama katika Mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla.

Mungure amesema gari hilo lilikuwa miongoni mwa nyenzo muhimu za chama katika kutekeleza shughuli zake, hivyo kutokuwepo kwake kumeathiri baadhi ya majukumu ya kiutendaji.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha halijatoa taarifa rasmi kuhusu tuhuma zinazomkabili Ndonde wala hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi yake.

Kwa upande wake Ndonde alipohojiwa  alikiri kujaribu kuiba mali hizo za chama kwa madai kwamba anakidai chama chake hicho cha zamani kiasi cha shilingi milioni 6 kama posho aliyostahili kulipwa wakati anakitumikia

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم