Ad
Breaking🔥

LUKUMAY ATAKA KANISA LISHIRIKIANE NA SERIKALI KUHUBIRI AFYA YA UMMA

LUKUMAY ATAKA KANISA LISHIRIKIANE NA  SERIKALI KUHUBIRI AFYA YA UMMA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesema Kanisa lina wajibu mkubwa wa kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu afya ya umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu kwa wakati.
Dkt. Lukumay alisema hayo leo Septemba 25,2026  jijini Arusha wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) unaofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Engarenarok.

Alisema pamoja na Kanisa kuwa na jukumu la kuhubiri neno la Mungu na kuimarisha imani za waumini, lina wajibu pia wa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya na matumizi ya huduma za matibabu.





“Pamoja na umoja ambao Askofu ameujenga katika kanisa, ni wajibu wa kanisa pia kuhubiri afya ya umma. Kama hakuna afya njema, ni vigumu sana kumwamini Mungu,” alisema Dkt. Lukumay.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo katika sekta ya afya, ikiwamo kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wenye mahitaji mbalimbali.

Dkt. Lukumay, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, alisema mbunge hana wajibu wa kutunga sheria na kupitisha bajeti pekee, bali anatakiwa pia kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali na kusikiliza changamoto za wananchi.

“Kazi kubwa ya Bunge ni kutunga sheria, kupanga bajeti na kuisimamia Serikali, lakini pia tunawajibika kuwasimamia watu wetu. Mimi nasimama hapa kusema niko kwa ajili hiyo,” alisema.

Alitoa mfano wa mtoto mwenye tatizo la moyo ambaye familia yake haikuwa na uwezo wa kugharamia matibabu, akisema baada ya kuona taarifa kuhusu mtoto huyo kwenye mitandao ya kijamii, alifuatilia suala hilo na kufika nyumbani kwa familia hiyo.

Dkt. Lukumay alisema hatua zilizochukuliwa ziliwezesha mtoto huyo kufikishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam ambako alipata matibabu.

Alisema awali wananchi walikuwa wamechangisha fedha kwa ajili ya kumsaidia mtoto huyo, lakini kiasi kilichopatikana hakikutosha kukidhi gharama zilizohitajika kwa matibabu.

“Nilichofanya kama mbunge wao na Serikali yetu sikivu ni kumchukua yule mtoto akapelekwa kutibiwa na amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Jakaya Kikwete,” alisema.

Dkt. Lukumay alisema tukio hilo linaonyesha umuhimu wa viongozi kuwa karibu na wananchi na kushirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili, hasa katika sekta ya afya.

Alisema pia amekuwa akitumia nafasi mbalimbali kutafuta ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo, akitaja congenital heart disease kama miongoni mwa changamoto zinazohitaji uwekezaji na utaalamu zaidi.

Kwa upande mwingine, Dkt. Lukumay aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za afya, akisema juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na taasisi za dini na wadau wengine ili wananchi wapate huduma bora.

Akizungumzia uhusiano kati ya Serikali na Kanisa, alisema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa taasisi za dini zinachangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za kijamii, hususan afya na elimu.

Aliwataka viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi na kuimarisha amani na upendo nchini.

“Tuendelee kupenda nchi yetu, tuendelee kuiombea amani nchi yetu kwa sababu hakuna nchi nyingine tuliyonayo. Tunayo Tanzania moja,” alisema.

Dkt. Lukumay pia alimpongeza Askofu Dkt. Godson Abel Mollel kwa uongozi wake na juhudi za kuimarisha umoja wa waumini ndani ya Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Alisema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye umoja, upendo na mshikamano, akiahidi kuendelea kushirikiana na Kanisa katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Arusha na maeneo mengine.

Mkutano Mkuu wa 27 wa Dayosisi ya Kaskazini Kati unaendelea katika Kanisa la KKKT Usharika wa Engarenarok jijini Arusha, ukihusisha Maaskofu,wachungaji, viongozi mbalimbali akiwemo waziri wa habari ,utamaduni ,sanaa na Michezo ,Paulo Makonda ,Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya Dayosisi hiyo.





Ends

Post a Comment

أحدث أقدم