Ad
Breaking🔥

NECTA YABADILI KIA ANGANI MITIHANI YA KIDATO CHA NNE,ELNINO YATIBUA MIPANGO

NECTA YABADILI RATIBA YA MITIHANI KUEPUKA MVUA ZA EL NIÑO

Na Joseph Ngilisho | Arusha

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limebadili ratiba ya baadhi ya mitihani na upimaji wa kitaifa uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba na Novemba 2026, kutokana na tahadhari ya uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa za El Niño.

Mabadiliko hayo yamefanywa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi wa mitihani na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

Akizungumza jana, Ijumaa, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alisema Wizara imepokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa.

Alisema baada ya kutathmini hali hiyo, Wizara imeona umuhimu wa kurekebisha ratiba ya uendeshaji wa Upimaji na Mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026 ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.

“Lengo la marekebisho ya ratiba ni kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka za mitihani iwapo mvua kubwa zitatokea mwezi Novemba 2026,” alisema.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne umehamishwa kutoka Oktoba 21 na 22 na sasa utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, ambao awali ulipangwa kufanyika Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.

Katika mabadiliko hayo, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili nao umehamishwa kutoka Novemba 2 hadi 13 na sasa utafanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 23, 2026.

Kwa upande wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kufanyika kuanzia Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6, 2026.

NECTA imesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha shughuli za mitihani zinafanyika katika mazingira salama na yenye udhibiti wa changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم