Ad
Breaking🔥

BOTI YAZAMA 40 WAFARIKI DUNIA,49 WAOKOLEWA

BOTI YA KIGOMA–KALEMIE YAZAMA, 41 WAFARIKI

Na ArushaDigital 

KIGOMA. Watu 41 wamefariki dunia na wengine 49 wameokolewa baada ya boti iliyokuwa ikisafiri kutoka Kigoma nchini Tanzania kuelekea Kalemie, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuzama katika Ziwa Tanganyika.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mapera, karibu na Kabimba, upande wa DRC, wakati chombo hicho kikielekea Kalemie kikitokea Kigoma. Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Tanganyika, Norris Mulongoyi, takriban watu 100 walikuwa ndani ya boti hiyo pamoja na shehena ya mizigo.

Mulongoyi alisema juhudi za uokoaji zinaendelea katika Ziwa Tanganyika, huku vikosi vya uokoaji vikifanya msako kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa boti hiyo, inayotajwa kwa jina la MV MJP, ilianza kuelemea upande mmoja kabla ya kuzama katika maji ya Ziwa Tanganyika. Hata hivyo, chanzo rasmi cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa na uchunguzi zaidi unatarajiwa kubaini kilichosababisha chombo hicho kupinduka.

Ajali hiyo imeibua pia maswali kuhusu kiwango cha mzigo uliokuwa ndani ya boti hiyo. Baadhi ya taarifa za eneo la tukio zimedai kuwa chombo hicho kilikuwa kimebeba zaidi ya tani 480 za unga wa ngano pamoja na magari manne, huku uwezo wake wa mzigo ukitajwa kuwa tani 550.

Hata hivyo, mamlaka hazijathibitisha kuwa mzigo huo ndio uliosababisha ajali, na uchunguzi ndio utakaobaini iwapo kulikuwa na ukiukwaji wa viwango vya usalama au uwezo wa chombo hicho.

Baadhi ya manusura walieleza kuwa abiria walikuwa wamelala wakati boti ilipoanza kuelemea upande mmoja kabla ya kuzama, huku shughuli za uokoaji zikifanyika baada ya tukio.

Ajali hiyo imeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika, ambalo hutumiwa kwa kiasi kikubwa kusafirisha abiria na mizigo kati ya Tanzania na DRC.

Taarifa zaidi kuhusu idadi ya waliopotea na chanzo cha ajali zinatarajiwa kutolewa kadiri shughuli za utafutaji na uchunguzi zitakavyoendelea.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم