Ad
Breaking🔥

TAASISI ZA UMMA ZASIMAMIA UWEKEZAJI WA SH TRILIONI 120 KATIKA UCHUMI WA TAIFA,NDEJEMBI KUFUNGUA JUKWAA LA WENYEVITI WA BODI NA WAKURUGENZI WA MASHIRIKA YA UMMA ARUSHA

 TAASISI ZA UMMA ZASIMAMIA UWEKEZAJI WA SH TRILIONI 120 KATIKA UCHUMI WA TAIFA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

TAASISI na mashirika ya umma nchini Tanzania yanasimamia mali na uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya Sh120 trilioni, huku Serikali ikianza hatua mpya za kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuongeza mchango wa taasisi hizo katika uchumi wa taifa.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema hayo leo Septemba 25,2026 mjini Arusha wakati akielezea maandalizi ya Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakurugenzi Wakuu wa Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) linalotarajiwa kufunguliwa Jumatatu na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.


Mchechu alisema Tanzania ina takribani taasisi na mashirika ya umma 308, ambayo kwa pamoja yanasimamia rasilimali kubwa zinazohitaji uongozi madhubuti, uwajibikaji na mikakati ya kuhakikisha zinatumika kwa tija kwa manufaa ya wananchi.

“Taasisi tunazozizungumzia leo zinasimamia mtaji mkubwa. Tuna taasisi za umma zenye mali zinazozidi Sh120 trilioni,” alisema.

Alisema Serikali imeweka mkazo katika kuboresha utendaji wa taasisi hizo ili zisibaki kuwa tegemezi kwa fedha za Serikali, bali zijenge uwezo wa kujiendesha kibiashara, kuongeza mapato, kulinda mali za umma na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mchechu alisema taasisi mbili za umma zinatarajiwa kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua inayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuwezesha wananchi pamoja na wawekezaji kushiriki katika umiliki wake kupitia ununuzi wa hisa.

Alisema Serikali inaendelea kupitia utendaji wa mashirika na taasisi mbalimbali na kuzihamasisha zile zenye uwezo wa kibiashara kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji.

Kwa mujibu wa Mchechu, kuorodheshwa katika soko la hisa kutasaidia kuongeza uwazi katika uendeshaji na utoaji wa taarifa za kifedha, huku kukitoa fursa kwa wananchi kushiriki katika umiliki wa baadhi ya taasisi .

Mchechu alisema Serikali pia imeanza kuimarisha mfumo wa kutathmini utendaji wa taasisi za umma kupitia mikataba ya utendaji inayoweka malengo na viashiria vinavyopaswa kufikiwa na viongozi ndani ya kipindi maalumu.

Alisema kwa sasa taasisi 13 zinahusika katika mchakato wa tathmini unaolenga kubaini maendeleo ya utekelezaji wa mikataba hiyo, changamoto zinazokabili taasisi hizo na maeneo yanayohitaji maboresho.

Alitolea mfano Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na taasisi nyingine zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi, akisema Serikali inaendelea kutafuta namna ya kuhakikisha taasisi hizo zinafanya kazi kwa ufanisi huku zikiendelea kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma kwa umma.

“Kila mwaka tunaingia mikataba ya utendaji na taasisi na kufuatilia utekelezaji wake. Mwenyekiti wa taasisi anasaini makubaliano hayo, na sisi tunafuatilia kuhakikisha kile tulichokubaliana kinatekelezwa,” alisema.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa na uwekezaji unaelekezwa katika maeneo yanayoweza kuzalisha manufaa yanayoonekana kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Mchechu alisema zaidi ya washiriki 700 wanatarajiwa kushiriki katika jukwaa hilo litakalojadili uwekezaji katika sekta ya umma, maendeleo ya uchumi na nafasi ya taasisi za umma katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

Alisema kukutana kwa wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wakuu kutatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa taasisi zinazomiliki na kusimamia rasilimali za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha , Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, alisema Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kufungua jukwaa hilo Jumatatu kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Makalla alisema jukwaa hilo ni muhimu kwa kuwa linawakutanisha viongozi wakuu wa taasisi zinazochangia katika uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma mbalimbali, hivyo kuwa nafasi ya kujadili namna ya kuongeza mchango wao katika uchumi wa taifa.

Alisema mashirika ya umma yanapaswa kuoanisha mipango yao ya utendaji na vipaumbele vya maendeleo ya taifa ili kuhakikisha mipango hiyo inatafsirika katika programu zinazotekelezeka na matokeo yanayopimika.

“Jukwaa hili ni muhimu kwa sababu mashirika ya umma yanatoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kupitia uzalishaji, shughuli za biashara na utoaji wa huduma mbalimbali,” alisema.

Makalla pia aliwataka wakazi na wafanyabiashara wa Arusha, hususan wanaofanya shughuli za hoteli, usafiri, burudani na huduma nyingine, kutumia ujio wa washiriki hao kama fursa ya kukuza shughuli zao na kuhakikisha wageni wanapata huduma bora.

Aliwahimiza washiriki wa jukwaa hilo kutumia muda wao kutembelea vivutio vya utalii vya mkoa huo, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Alisema hatua hiyo itaongeza fursa ya wageni kufahamu vivutio vya Tanzania na kupata uzoefu wa moja kwa moja wa utalii wa kaskazini mwa nchi.

Ends



Post a Comment

أحدث أقدم