Breaking🔥

LUKUMAY AMBANA KASEKENYA MIRADI YA BARABARA ARUMERU MAGHARIBI

LUKUMAY AMKUMBUSHA KASEKENYA MIRADI YA BARABARA ARUMERU

NA JOSEPH NGILISHO | DODOMA

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amefanya mazungumzo mafupi ndani ya viunga vya Bunge na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, akimkumbusha kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara inayotekelezwa katika jimbo hilo.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Septemba 1, 2026, Dkt. Lukumay alieleza umuhimu wa Serikali kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati, hususan barabara ya Mianzini–Ngaramtoni yenye urefu wa kilomita 18, inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Dkt. Lukumay alimkumbusha Naibu Waziri kuhusu ziara yake ya kukagua barabara hiyo Januari 2026, ambapo mkandarasi alieleza kuwa ujenzi huo ungetarajiwa kukamilika Juni au Julai 2026.

Kutokana na muda huo kupita, Mbunge huyo alitaka kufahamu mikakati ya Serikali kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua, akisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Dkt. Lukumay alitumia mazungumzo hayo kumkumbusha Naibu Waziri kuhusu barabara ya Sambasha–Olmotonyi–Ngaramtoni, yenye urefu wa kilomita 5.1, ambayo tayari imefanyiwa usanifu.

Alimuuliza Naibu Waziri ni lini Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara hiyo, ambayo wananchi wamekuwa wakisubiri utekelezaji wake.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Kasekenya alimhakikishia Dkt. Lukumay kuwa Serikali inazifanyia kazi hoja zote mbili na kwamba atampatia majibu kuhusu hatua zinazochukuliwa kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano huu wa Bunge.

Mazungumzo hayo yanaongeza msukumo wa uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu katika Jimbo la Arumeru Magharibi, huku wananchi wakisubiri kukamilika kwa barabara hizo zitakazosaidia kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post