ZARA TANZANIA YANG’ARA AFRIKA, YANYAKUA TUZO YA MWAKA WA PILI MFULULIZO


ZARA TANZANIA YANG’ARA AFRIKA, YANYAKUA TUZO YA MWAKA WA PILI MFULULIZO

Na Joseph Ngilisho | ZANZIBAR 

KAMPUNI ya Zara Tanzania Adventures imeendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya utalii wa dunia baada ya kutwaa tuzo ya Mwongoza Watalii Bora wa Matukio ya Kusisimua Afrika 2026 (Africa’s Leading Adventure Tour Operator 2026) katika tuzo za kimataifa za World Travel Awards.


Ushindi huo umeifanya Zara Tanzania Adventures kutwaa tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya pia kuibuka mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2025.

Katika taarifa yake, kampuni hiyo imeeleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja za timu yake, wakiwemo waongoza watalii wa milimani, wapagazi, waongoza safari za wanyamapori, madereva, wafanyakazi wa hoteli na kambi pamoja na watumishi wanaofanya kazi nyuma ya pazia.

“Tunajivunia sana kutangaza kwamba Zara Tanzania Adventures imetajwa kuwa Mwongoza Watalii Bora wa Matukio ya Kusisimua Afrika 2026 na World Travel Awards,” ilieleza kampuni hiyo.

Zara Tanzania Adventures ilisema ushindi huo una umuhimu mkubwa zaidi kwa kuwa imefanikiwa kutetea taji ililolitwaa mwaka 2025, jambo linaloendelea kuonyesha nafasi yake katika ushindani wa soko la utalii barani Afrika.

Kampuni hiyo pia imewashukuru watalii na washirika wake kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa kuendelea kuiamini, kuiunga mkono na kuchagua Tanzania kama moja ya vivutio vyao vya utalii.

“Kuanzia kileleni mwa Mlima Kilimanjaro hadi kwenye tambarare za Serengeti, tutaendelea kuunda safari na matukio yasiyosahaulika huku tukiendelea kuwaunga mkono watu wetu, jamii na mazingira,” ilisema taarifa hiyo.

Ushindi huo unatajwa kuwa chachu zaidi kwa Tanzania katika kuendelea kujitangaza kimataifa kama moja ya nchi zenye vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Serengeti na maeneo mengine yenye vivutio vya asili.

Tuzo za World Travel Awards ni miongoni mwa tuzo zinazotambulika katika sekta ya usafiri na utalii duniani, huku ushindi wa Zara Tanzania Adventures kwa miaka miwili mfululizo ukiendelea kuongeza heshima kwa kampuni hiyo na tasnia ya utalii nchini.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post