MKUDE AITAKA TRA KUONDOA KERO, WALIPA KODI WAPEWE HUDUMA BORA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modestin Mkude, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuondoa kero kwa wafanyabiashara na kuboresha huduma kwa walipa kodi, huku akiwaagiza wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari.
Mkude alisema hayo leo Agosti 29,2026 jijini Arusha wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, katika hafla ya TRA ya kutambua na kuthamini mchango wa walipa kodi na wadau mbalimbali.
Alisema mazingira mazuri ya biashara na huduma bora kwa walipa kodi ni muhimu katika kuongeza ari ya wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao kwa hiari na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
“Ondoeni kero ndogondogo kwa wafanyabiashara, toeni huduma bora kwa wakati, tuepuke usumbufu usio wa lazima na tuendelee kutoa elimu ili kujenga uelewa na hali ya kulipa kodi,” alisema Mkude.
Aliwataka wafanyabiashara kujisajili, kulipa kodi kwa usahihi, kudai na kutoa risiti pamoja na kutoa taarifa kuhusu ukwepaji kodi na biashara za magendo.
“Kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Tuna miradi mingi ya kitaifa na kimkoa ambayo yote inategemea kodi. Tunapolipa kodi tunaonyesha uzalendo na uwajibikaji kama Watanzania,” alisema.
Arusha yavuka lengo
Mkude aliipongeza TRA Mkoa wa Arusha kwa kuvuka lengo la makusanyo katika mwaka wa fedha 2022/2023, ambapo ililenga kukusanya Sh bilioni 504.71 na kufanikiwa kukusanya Sh bilioni 519.64, sawa na asilimia 103 ya lengo.
Alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuongezeka kwa uelewa wa wafanyabiashara kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi na umuhimu wa mapato hayo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema pia amekuwa akikutana na wafanyabiashara wanaojivunia kujitambulisha kuwa ni walipa kodi, akisema hali hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu wajibu wao kwa taifa.
“Wameanza kuelewa kwamba ni wajibu wao wa msingi na hawana aibu kusema sisi ni walipa kodi mbele ya viongozi na watu wengine. Huo ni mfano mzuri na ishara nzuri,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Ted Silkuwasha, akimwakilisha Kamishna wa Kodi wa TRA nchini, aliipongeza Arusha kwa kuwa miongoni mwa mikoa muhimu katika ukusanyaji wa mapato, akisema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Serikali, TRA, wafanyabiashara na walipa kodi.
Silkuwasha alisema Arusha ina nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na shughuli zake za madini, kilimo, biashara na sekta nyingine za uzalishaji.
“Ni heshima kubwa sana kwa Mkoa wa Arusha. Jukumu hili si rahisi kulifikia bila kuwa na ushirikiano kati ya wafanyabiashara, Serikali ya Mkoa na Mamlaka ya Mapato kwa ujumla wake,” alisema.
Alisema TRA inathamini walipa kodi wanaotekeleza wajibu wao kwa hiari, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ndio unaowezesha mamlaka hiyo kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.
“Tunawashukuru zaidi walipa kodi ambao wanakuwa na moyo wa kulipa na mapenzi kwa taifa lao. Wanapotoa kwa hiari, hata mapato yetu yanakuwa yanatimia,” alisema.
Silkuwasha aliomba ushirikiano kati ya TRA, Serikali ya Mkoa, wafanyabiashara na walipa kodi kuendelea, akisema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yanahitaji mahusiano mazuri na mazingira rafiki kwa walipa kodi.
“Tunashukuru kwa ushirikiano ambao tunaupata kutoka mkoa huu, kutoka kwa wafanyabiashara na kutoka kwa walipa kodi wote. Tunapenda kuomba kwamba ushirikiano huu uendelee,” alisema.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, aliwataka viongozi na watendaji wa TRA kuhakikisha taasisi hiyo haisogei nyuma, bali inaendelea kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa.
Dkt. Nguvila alisema maendeleo ya nchi hayawezi kutenganishwa na uwezo wa Serikali kukusanya mapato ya ndani, akisisitiza kuwa TRA ikiwa na ufanisi zaidi, Taifa litaongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tutaendelea kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba taasisi hii ya TRA hairudi nyuma bali isonge mbele. Kwa sababu tukisonga mbele tutapata maendeleo, tukisonga mbele tutapata mafanikio,” alisema.
Alisema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha itaendelea kushirikiana na TRA pamoja na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa.
Dkt. Nguvila pia aliwataka watumishi wa Serikali kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mkude aliwataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kushirikiana na TRA kwa kutoa taarifa wanapobaini vitendo vya ukwepaji kodi, magendo au ukiukwaji mwingine wa sheria za kodi.
Aliwataka pia wafanyabiashara kuwasiliana na TRA wanapokumbana na changamoto ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Aidha, aliipongeza TRA kwa ubunifu wa kutumia njia mbalimbali kuhamasisha ulipaji wa kodi, akitolea mfano matumizi ya mpira wa TRA katika kueneza ujumbe wa ulipaji kodi.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na TRA kuhakikisha inafikia malengo yake, huku ikiweka miundombinu na mazingira yatakayowawezesha wafanyabiashara kukuza shughuli zao na kuongeza mchango wao katika uchumi.
Ends





Post a Comment