WMA YAJIVUNIA UTEKELEZAJI WA ASILIMIA 92, NAIBU WAZIRI KUZINDUA DIRA MPYA YA MIAKA MITANO ARUSHA.

WMA YAJIVUNIA UTEKELEZAJI WA ASILIMIA 92, NAIBU WAZIRI KUZINDUA DIRA MPYA YA MIAKA MITANO ARUSHA.

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umeibuka na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa mipango yake kwa kufikia asilimia 92 katika mwaka wa fedha uliopita, huku ukitangaza kuingia katika hatua mpya ya mageuzi ya utendaji kupitia uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano, unaolenga kuimarisha usimamizi wa vipimo, kuongeza matumizi ya teknolojia na kuboresha huduma kwa wananchi.

Mafanikio hayo yanakuja wakati taasisi hiyo ikijiandaa kufanya Kikao cha 38 cha Baraza la Wafanyakazi kesho jijini Arusha, kikao kitakachotathmini utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka uliopita, kupima mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika mwaka mpya wa fedha.

Katika hatua inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya taasisi hiyo, Mbunge na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Lazaro Londo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuzindua Mpango Mkakati wa WMA wa miaka mitano, unaotajwa kuwa dira ya kuifanya taasisi hiyo iendane na kasi ya mageuzi ya kidijitali na mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Akizungumza kuelekea kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Mark Kihula, amesema mafanikio yaliyopatikana si ya bahati mbaya, bali ni matokeo ya utekelezaji madhubuti wa mipango ya taasisi na ushirikiano wa wafanyakazi katika kuhakikisha huduma za vipimo zinakuwa bora, za kuaminika na zenye tija kwa uchumi wa Taifa.

"Tumefanikiwa kutekeleza mpango wetu kwa takribani asilimia 92. Hii ni hatua kubwa inayodhihirisha dhamira ya taasisi katika kusimamia matumizi sahihi ya vipimo, kuongeza uwazi katika biashara na kuboresha huduma kwa wananchi," amesema Kihula.

Amesema katika kipindi hicho, WMA imeongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa, hatua iliyorahisisha usimamizi wa shughuli za vipimo, kuongeza ufanisi wa kazi na kupunguza mianya ya udanganyifu katika biashara.

Mbali na hilo, taasisi hiyo imeongeza makusanyo ya mapato, kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha motisha kwa watumishi kupitia posho na maboresho mengine yanayolenga kuongeza ari ya kazi na uwajibikaji.

Kihula amesema Baraza la Wafanyakazi linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga taasisi yenye uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya maendeleo ya WMA.

"Tutatumia kikao hiki kutathmini tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Lengo ni kuhakikisha kila mpango tunaouweka unaleta matokeo yanayogusa wananchi na kuchochea maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda," amesema.

Ameeleza kuwa kabla ya kikao hicho, wajumbe wapya wa Baraza la Wafanyakazi walipatiwa mafunzo kuhusu majukumu yao, sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi yenye tija kwa taasisi.

Kwa mujibu wa WMA, utekelezaji wa Mpango Mkakati mpya utaongeza kasi ya matumizi ya teknolojia, kuimarisha ukaguzi wa vipimo katika sekta mbalimbali za uchumi, kulinda haki za walaji na wafanyabiashara, pamoja na kuongeza mchango wa taasisi hiyo katika kujenga mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki na uchumi imara.

Viongozi wa WMA wanaamini kuwa mafanikio yaliyopatikana katika mwaka uliopita ndiyo msingi wa kuijenga taasisi hiyo kuwa miongoni mwa taasisi za umma zinazoongoza kwa ubunifu, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa Watanzania.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post