KKMK YAANZA KUANDAA MUSWADA WA MFANO WA MARIDHIANO YA TAIFA
By Arushadigital-DAR ES SALAAM
Mchakato wa kuelekea maridhiano na muafaka wa kitaifa umeingia hatua mpya baada ya Kamati ya Kusukuma Maridhiano ya Kitaifa (KKMK) kutangaza kuanza rasmi maandalizi ya Muswada wa Mfano (Model Bill) utakaoweka mfumo wa kisheria na kiutawala wa kuendesha mazungumzo ya maridhiano nchini.
Hatua hiyo inalenga kuweka msingi wa mazungumzo yatakayosaidia kuimarisha umoja wa taifa, kurejesha uelewano miongoni mwa wadau mbalimbali na kuweka mazingira yanayodaiwa kuwa muhimu kabla ya kuanza mchakato wa uandishi wa Katiba mpya.
Katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa KKMK, Odero Charles Odero, kamati hiyo imesema maandalizi ya muswada huo yamechochewa na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na Jaji Chande kuhusu umuhimu wa mazungumzo ya maridhiano kama njia ya kuponya taifa na kujenga mwafaka wa kitaifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, muswada huo unakusudiwa kuweka mfumo rasmi wa uendeshaji wa mazungumzo, ikiwemo utaratibu wa uteuzi wa wajumbe, ajenda za mazungumzo, muundo wa tume itakayosimamia mchakato huo pamoja na majukumu ya wadau wote watakaoshiriki.
Aidha, muswada huo utaweka misingi ya ushirikishwaji wa wananchi, taasisi za umma na binafsi, vyama vya siasa, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuhakikisha mchakato unakuwa shirikishi na wenye uwazi.
KKMK pia imeeleza kuwa muswada huo utaweka utaratibu wa utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa, kulinda misingi ya haki, uwazi, uwajibikaji na umoja wa kitaifa, pamoja na kuainisha mfumo wa fidia kwa waathirika wa migogoro au matukio yatakayohusishwa na mchakato wa maridhiano.
Kamati hiyo imesema kabla ya kukamilisha muswada huo, itafanya mashauriano mapana na wadau wa kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha maoni ya wananchi yanajumuishwa kikamilifu.
"Tunatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kwa amani, uwazi na uzalendo katika kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kujenga taifa lenye mshikamano, haki na maridhiano ya kudumu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
KKMK imeongeza kuwa mchakato huo haupaswi kutazamwa kama ajenda ya kisiasa pekee, bali ni jukumu la kitaifa lenye lengo la kuimarisha amani, umoja na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kamati hiyo imesema ratiba ya mashauriano pamoja na utaratibu wa kuwasilisha maoni ya wananchi itatangazwa rasmi kupitia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya umma katika siku zijazo.
Ends

Post a Comment