WAZAZI WAIOMBA SERIKALI KUTOA MUDA WA MAANDALIZI KABLA YA UTEKELEZAJI WA MITAALA MIPYA
Na Hadija Bagasha | Tanga
WAZAZI mkoani Tanga wameiomba Serikali kuhakikisha wanafunzi, walimu na wazazi wanapewa muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mabadiliko ya mitaala ya elimu, wakionya kuwa utekelezaji wa haraka, hasa wakati wanafunzi wakielekea kwenye mitihani, unaweza kuathiri ufaulu wao.
Wamesema kuwa, pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya elimu, utekelezaji wa mitaala mipya unapaswa kufanyika kwa maandalizi ya kutosha ili kuondoa mkanganyiko unaoweza kuwakumba wanafunzi na walimu.
Kauli hiyo ilitolewa katika mkutano wa wazazi wa wanafunzi wa Kidato cha Pili uliofanyika katika Shule ya Sekondari Mwapachu, jijini Tanga, ambapo wazazi walieleza wasiwasi wao kuhusu muda mfupi uliobaki kabla ya mitihani huku kukiwa na mabadiliko ya mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji.
Mmoja wa wazazi, Lucy Faustine, alisema wanafunzi wanaokaribia kufanya mitihani wanahitaji utulivu wa kujifunza badala ya kuanza kuzoea mfumo mpya wa elimu katikati ya mwaka wa masomo.
"Kinachotupa wasiwasi ni kuona watoto wamebakiza muda mfupi kuelekea mitihani, lakini tayari wameanza kupitia mabadiliko ya mtaala. Hatujui kama wataweza kuendana na mfumo huo mpya na kufanya vizuri katika mitihani yao," alisema.
Aliishauri Serikali kutangaza mapema mabadiliko ya mitaala na kuanza utekelezaji wake mwanzoni mwa mwaka wa masomo ili wanafunzi waanze safari yao ya elimu katika mfumo mmoja.
"Iwapo kuna mtaala mpya, ni vyema utekelezaji wake ukaanza Januari. Hii itawapa wanafunzi nafasi ya kuzoea mfumo huo tangu mwanzo badala ya kubadilishiwa utaratibu katikati ya mwaka," alisema.
Lucy alisema pia wazazi wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko hayo ili waweze kuwasaidia watoto wao nyumbani na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma kwa ufanisi.
Aidha, aliitaka Serikali kuunda timu za wataalamu wa elimu zitakazotembelea shule mbalimbali nchini kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa mitaala mipya, kuwajengea uwezo walimu na kujibu maswali ya wazazi na wanafunzi.
"Wataalamu hao wawe karibu na shule, waendeshe semina na mikutano ya mara kwa mara ili kila mdau aelewe mabadiliko haya. Hilo litawasaidia watoto kujifunza kwa utulivu na kujiamini zaidi," alisema.
Wazazi hao walisisitiza kuwa mafanikio ya mabadiliko yoyote katika sekta ya elimu yanategemea ushirikishwaji wa wadau wote na maandalizi ya kutosha kabla ya utekelezaji wake.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Tanzania for Education, Yusuf Ugutu, aliwahimiza wazazi kuendelea kusimamia lishe bora, mahudhurio na maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao, akieleza kuwa ushirikiano kati ya familia na shule ni msingi wa kuongeza ufaulu.
Ugutu alisema watoto wanaopata lishe bora, mazingira mazuri ya kujifunza na motisha kutoka kwa wazazi wao wana nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri katika masomo na kufikia malengo yao ya kielimu.
Ends..



Post a Comment