UVCCM ARUMERU YAMPONGEZA NDEJEMBI, YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWAAMINI VIJANA

UVCCM ARUMERU YAMPONGEZA NDEJEMBI, YAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWAAMINI VIJANA

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Arumeru umempongeza Dkt. Deogratias Ndejembi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukisema uteuzi huo ni ushahidi wa imani ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vijana.

Aidha, jumuiya hiyo imemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwapa vijana nafasi za uongozi na kumtaka aendelee kuwaamini kwa kuwapa majukumu makubwa katika ujenzi wa Taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Agosti 28,2026 na viongozi wa UVCCM  Wilaya ya Arumeru, wakizungumza na waandishi wa habari baada ya vikao vya Kamati za Utekelezaji vya wilaya hiyo vilivyokutana kujadili na kutoa msimamo kuhusu uteuzi wa Dkt. Ndejembi.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Arumeru, Lempapa Lukumay, amesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwa vijana na jumuiya hiyo, kwa kuwa Dkt. Ndejembi ni zao la UVCCM ambaye amepitia misingi ya malezi ya kisiasa na kiuongozi ndani ya jumuiya hiyo.

“Tunampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha imani kubwa kwa vijana. Dkt. Ndejembi ni zao la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi na ametokana na Baraza la Umoja wa Vijana. Uteuzi wake ni ishara kwamba vijana wanaweza kuaminiwa na kupewa nafasi kubwa katika uongozi wa nchi,” amesema Lukumay.

Amesema hatua hiyo inapaswa kuwa chachu kwa vijana wengine ndani na nje ya CCM kujenga uwezo, kujituma na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na Taifa ili kuwa tayari kushika dhamana mbalimbali za uongozi.

Lukumay pia amewapongeza wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM kwa kuunga mkono jina la Dkt. Ndejembi, huku akilipongeza Bunge kwa kumpitisha kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa Taifa.

Amesema UVCCM Arumeru inaamini Dkt. Ndejembi atatekeleza majukumu yake kwa uadilifu na ufanisi, huku akimtaka awe mfano kwa vijana wengine wanaotarajia kushika nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Arumeru, Ally Sululu, amesema uteuzi wa Dkt. Ndejembi ni uthibitisho kwamba vijana wanaweza kuaminiwa na kupewa dhamana kubwa wanapojenga uwezo na kuwa tayari kulitumikia Taifa.

Sululu amesema Ndejembi ni zao la UVCCM nchini, akieleza kuwa amepitia hatua mbalimbali za malezi ya kisiasa na kiuongozi ndani ya jumuiya hiyo kabla ya kufikia nafasi kubwa ya kitaifa.

“Tunampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuonyesha imani kwa vijana na kumpa dhamana mwenzetu Deogratias Ndejembi. Ndejembi ni zao la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi nchini,” amesema Sululu.

Amesema uteuzi huo ni faraja kwa vijana waliopo ndani ya UVCCM kwa kuwa unaonyesha kuwa ushiriki katika shughuli za chama, kujenga uwezo na kujituma kunaweza kuwaandaa vijana kushika nafasi kubwa za uongozi.

Sululu amemuomba Rais Samia aendelee kuwaamini vijana na kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi, huku akimtakia hekima na nguvu katika kuliongoza Taifa.

Naye Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa CCM Wilaya ya Arumeru, Erick Jeremiah, amesema vijana wa CCM wamepokea uteuzi huo kwa furaha na wako tayari kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa majukumu yake.

Jeremiah amesema uteuzi wa Dkt. Ndejembi, kijana mwenye umri wa miaka 43, ni ujumbe kwa vijana wengine kwamba wanaweza kuaminiwa na kupewa dhamana kubwa katika uongozi wa Taifa.

“Vijana tupo na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunampongeza kwa kutuamini vijana, kwa kumteua kijana mwenye miaka 43 katika nafasi ya juu kabisa ya nchi ya Makamu wa Rais,” amesema Jeremiah.

Amesema uteuzi huo unapaswa kuwa chachu kwa vijana kujituma zaidi katika shughuli za chama na Taifa, akiahidi kuwa vijana wa CCM wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha imani ambayo Rais Samia ameendelea kuwa nayo kwa vijana.

“Tupo nyuma yake, tunapigia kazi na tunahakikisha kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kuwaamini vijana wengine wengi zaidi,” amesema.

Viongozi hao kwa pamoja wamewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na ushirikiano, wakisema mazingira hayo ni muhimu katika kuhakikisha Taifa linaendelea kusonga mbele na kutekeleza miradi ya maendeleo.

UVCCM Arumeru pia imemtakia Dkt. Ndejembi kila la heri katika majukumu yake mapya, ikisema inaamini atatumia nafasi hiyo kuitumikia Tanzania kwa uadilifu na kuendeleza misingi ya uongozi aliyojengewa ndani ya UVCCM.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم