NAIBU WAZIRI MAHMOUD AITAKA RSA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUPUNGUZA AJALI NCHINI
....Aitaka matokeo ya elimu ya usalama barabarani, mabalozi wasijichukulie mamlaka ya polisi
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mahmoud, amelitaka baraza la usalama barabarani (RSA) Tanzania kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ajali za barabarani, lakini ameweka masharti mazito ya uwajibikaji, weledi, nidhamu na uwezo wa kuonesha matokeo ya kazi zake.
Mahmoud alisema hayo,Agosti 30,2026 wakati akifunga Wiki ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), akisema Serikali kupitia Baraza la Taifa la Usalama Barabarani iko tayari kushirikiana na RSA Tanzania, lakini ushirikiano huo lazima uzingatie weledi, uwajibikaji, uwezo na matokeo yanayopimika.Alisema Baraza na taasisi husika zitapitia maeneo ambayo RSA Tanzania inaweza kushirikishwa katika utekelezaji wa majukumu ya usalama barabarani, huku akitaka taasisi hiyo kuweka wazi maeneo inayolenga kufanya kazi, makundi inayoweza kuyafikia na matokeo inayotarajia kuyapata.
KANZIDATA YA MABALOZI
Naibu Waziri aliitaka RSA Tanzania kuandaa kanzidata ya mabalozi wake ikionesha maeneo wanakotoka, taaluma na mafunzo waliyopata, ili wapatiwe mafunzo kulingana na mahitaji.
Alisema mabalozi wenye taaluma za sheria, afya, elimu, uhandisi na fani nyingine washirikishwe kutumia utaalamu wao katika kujenga elimu bora ya usalama barabarani.
Aliitaka RSA kuweka vipaumbele kwa kuchagua maeneo na makundi yenye uhitaji mkubwa badala ya kujaribu kufanya kila jambo kwa wakati mmoja.
MABALOZI WASIJICHUKULIE MADARAKA
Mahmoud aliwakumbusha mabalozi kuwa hawana mamlaka ya kusimamisha magari, kutoa adhabu wala kuingilia utekelezaji wa sheria.
“Mabalozi wanapaswa kufahamu kuwa wao si maafisa wa usalama barabarani wala waamuzi wa mamlaka za udhibiti,” alisema.
Aliwataka kulinda heshima ya jina la balozi na kulitumia kwa shughuli zinazolenga kuokoa maisha na kuongeza usalama barabarani.
MADEREVA, WAMILIKI WACHOMBEKE
Akizungumza na madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri, Mahmoud alisema usalama huanza na uamuzi wa mtu mmoja mmoja.
Aliwataka madereva kuepuka matumizi ya simu wakati wa kuendesha, ulevi, mwendo kasi na kutofunga mikanda, huku akiwataka kuendelea kupata mafunzo kwa kuwa teknolojia na sheria hubadilika.
Wamiliki wa vyombo vya usafiri, alisema, wasiwalazimishe madereva kukiuka sheria kwa ajili ya kutimiza malengo ya biashara.
“Malengo ya biashara yasitanguliwe mbele ya maisha na usalama wa wananchi,” alisema.
ABIRIA NAO WANAJUKUMU
Mahmoud aliwataka abiria kutomshawishi dereva kuongeza mwendo kwa sababu ya kuwahi, na kukataa kutumia huduma inayohatarisha maisha yao.
Pia aliwataka wazazi na walimu kuendelea kuwafundisha watoto matumizi salama ya barabara.
Alisema ajali si jukumu la Polisi pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi, Serikali, taasisi na asasi za kiraia.
RSA YATAKIWA KUJENGA USHIRIKIANO
Alisema RSA Tanzania, yenye zaidi ya wanachama 400, ina nafasi ya kusaidia Serikali kufikisha elimu kwa jamii na kutoa mrejesho wa changamoto za usalama barabarani.
Aliitaka kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi, TANROADS, TARURA, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, taasisi za elimu na wadau wa usafirishaji.
“Lengo letu si faida ya kibiashara, bali ni uhai wa watu, kupunguza ajali na kuleta uendeshaji ulio salama zaidi,” alisema.
Akizungumza kuhusu kaulimbiu “Zuia Ajali, Fanikisha Dira 2025,” alisema usalama barabarani ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa kwa kuwa ajali zinaathiri familia, nguvu kazi, huduma za afya na uchumi.
“Kuzuia ajali si jukumu la kikosi cha usalama barabarani pekee, ni wajibu wa kila taasisi na kila mwananchi,” alisema.
Ends




Post a Comment