Breaking🔥

MSAFIRI AFARIKI GHAFLA CHOONI STENDI NDOGO ARUSHA

MSAFIRI AFARIKI GHAFLA CHOONI STENDI NDOGO ARUSHA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MTU mmoja anayesadikiwa kuwa mkazi wa Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, amefariki dunia ghafla asubuhi ya leo, Agosti 4, 2026, baada ya kuanguka katika choo cha umma kilichopo Stendi Ndogo jijini Arusha, muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi lililokuwa limetoka Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio, marehemu aliwasili Stendi Ndogo akiwa na begi pamoja na mfuko, akidaiwa kuwa alikuwa akisafiri kuelekea Monduli. Inadaiwa aliingia kwenye daladala iliyokuwa ikielekea huko na kuacha mizigo yake ndani ya gari kabla ya kuomba kwenda kujisaidia.

Mashuhuda wamesema marehemu alikuwa akionekana akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa na alikuwa akitembea kwa shida, hali iliyowalazimu watu waliokuwa karibu kumpatia fimbo ili imsaidie kufika kwenye choo hicho.

Inaelezwa kuwa baada ya kuingia chooni, alikaa kwa takribani saa moja bila kutoka, jambo lililomfanya mhudumu wa choo kuingiwa na wasiwasi. Baada ya kugonga mlango mara kadhaa bila kupata majibu, mhudumu huyo alifungua mlango na kumkuta marehemu akiwa ameinama ndani ya choo.

Akizungumza baada ya tukio hilo, mhudumu huyo alisema alimtoa marehemu nje na kumkalisha kwenye kibaraza cha choo akiamini huenda angepata nafuu, lakini muda mfupi baadaye alianguka ghafla na kufariki dunia.

Tukio hilo lilivuta umati wa wasafiri na wananchi waliokuwa Stendi Ndogo kabla ya Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio, kuuzingira na kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi wa kubaini chanzo cha kifo ukiendelea.

Hadi kufikia wakati wa kuandikwa kwa taarifa hii, Jeshi la Polisi lilikuwa bado halijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, huku utambulisho kamili wa marehemu ukisubiri kuthibitishwa pamoja na matokeo ya uchunguzi.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم