Na Joseph Ngilisho | MONDULI
DIWANI wa Kata ya Monduli Mjini, Hussein Maasai, ameshambuliwa kwa makofi na ngumi usoni na Mwenyekiti wa Soko la Monduli, Josephat Mbilinyi, na kujeruhiwa vibaya katika jicho wakati akitekeleza majukumu yake ya kuzungumza na wafanyabiashara katika soko hilo.
Kwa mujibu wa Maasai, tukio hilo lilitokea jana Jumatano majira ya saa saba mchana, wakati akiwa katika eneo la soko akizungumza na wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Maasai alisema hakutarajia kukutana na shambulio hilo akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiuongozi na kwamba baada ya tukio hilo alikimbilia kituo cha polisi kutoa taarifa.
Baada ya taarifa hiyo kutolewa polisi, Mbilinyi alikamatwa na leo Alhamisi alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kudhuru mwili.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Jumatatu ijayo, huku Mbilinyi akiwa nje kwa dhamana.
Maasai alisema ameamua kuliachia suala hilo katika mikono ya vyombo vya sheria ili haki itendeke, akisisitiza kuwa hakutaka kulipiza kisasi baada ya kushambuliwa.
“Nilipata shambulio na kujeruhiwa mwili. Sikutarajia kwamba ningekutana na shambulio hilo. Lakini baada ya hapo nilitumia busara ya uongozi na kulifikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Alisema shambulio hilo lilimsababishia majeraha usoni, hususan katika eneo la jicho, na kwamba alikuwa akiendelea na matibabu.
Diwani huyo alisema alikuwa katika soko hilo kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuwafikia wananchi na wafanyabiashara, kusikiliza changamoto zao na kufuatilia masuala yanayohusu eneo lake la uwakilishi.
“Mimi ni diwani, ni utekelezaji wa majukumu yangu. Mimi ni mpokeaji wa changamoto za wananchi ambao wamenichagua. Hakuna sehemu yoyote katika eneo langu la kazi ambayo sina haki ya kufika kwa kutembelea wananchi ambao wamenichagua,” alisema.
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa tofauti za kisiasa kati yake na uongozi wa soko, Maasai alisema hakutaka kulizungumza kwa kina, akisisitiza kuwa ni vyema kusubiri mahakama itoe tafsiri na uamuzi wake.
“Mimi naendelea na majukumu yangu. Tusubiri mahakama itakavyotafsiri na kutoa haki,” alisema.
Kwa upande wake, Mbilinyi alisema alimpa makofi diwani huyo, akidai kitendo hicho kilichochewa na kutoshirikishwa kwake katika vikao vinavyofanywa na diwani huyo na wafanyabiashara wa soko.
Mbilinyi alisema viongozi wanapaswa kuheshimiana na kufuata utaratibu katika kushughulikia masuala ya wafanyabiashara, akidai diwani huyo amekuwa akifanya vikao bila kumshirikisha kama mwenyekiti wa soko.
Mbilinyi pia alisema mgogoro huo una mwelekeo wa kisiasa, akidai wakati wa kampeni za uchaguzi wa udiwani, Maasai aliahidi kuwa akichaguliwa angepunguza minada inayofanyika katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mbilinyi, kwa sasa kuna minada miwili inayofanyika Alhamisi na Jumapili, na diwani huyo aliahidi kuondoa mmoja ili kubaki mnada mmoja.
“Alipokuwa anagombea udiwani alisema akichaguliwa atafuta mnada mmoja kati ya miwili ili ubaki mmoja, kwa sababu minada hiyo inawafanya wafanyabiashara washindwe kuuza bidhaa zao sokoni,” alisema Mbilinyi.
Hata hivyo, Mbilinyi alisema diwani huyo amekuwa akiendeleza siasa katika utekelezaji wa majukumu yake, akidai pia kuna chuki za kisiasa zinazoathiri namna wanavyoshughulikia masuala ya soko.
Mbilinyi alisema pia aliitwa na polisi baada ya tukio hilo na kwenda kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.
Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Rukia Yusufu, alisema amesikitishwa na tukio hilo, akieleza kuwa alisikia kuhusu tukio hilo kupitia watu na kuahidi kulifuatilia.
Rukia alisema chama kitalishughulikia suala hilo mara baada ya kupokea taarifa rasmi.
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph, alisema amesikia kuhusu tukio hilo akiwa Dodoma na kulaani kitendo hicho.
Alisema tukio hilo ni baya na linaweza kukidhalilisha chama, huku akitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mhusika atakayebainika kuhusika na tukio hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Happiness Laizer, alisema amelisikia tukio hilo kutoka kwa watu, lakini hakuwa amepata taarifa kamili kuhusu kilichotokea.
Kwa sasa, suala hilo liko mikononi mwa vyombo vya sheria baada ya Mbilinyi kufikishwa mahakamani, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Jumatatu.
Maasai alisema ataendelea na matibabu na kutekeleza majukumu yake, huku akisisitiza kuwa amechagua njia ya kisheria badala ya kulipiza kisasi.
Ends.

إرسال تعليق