Breaking🔥

MILIONI 80 NA HEKA MOJA WALIZOAHIDIWA WANANCHI NANE ARUSHA WAFUTE KESI MAHAKAMANI ZAZUA BALAA,WENGINE WALILAMBA MIL. 40,WENGINE WAKAZUNGUKWA WAMO MADIWANI WASTAAFU.

FIDIA YA SH MILIONI 40, EKARI MOJA YAZUA MGOGORO

.....Wananchi nane wadai Sh milioni 80, eneo walilopewa halijaendelezwa — Diwani mstaafu ahoji chanzo cha fedha na utaratibu uliotumika...

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KIVUYO-Diwani Mstaafu 
OLOD-Diwani mstaafu

ARUSHA. Mgogoro wa muda mrefu wa umiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari 15 kati ya Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Huruma, kilichopo Muriet, Sokoni One jijini Arusha, na wananchi wanane, umeibuka upya baada ya kutotekelezwa kikamilifu kwa makubaliano yaliyolenga kumaliza kesi iliyodumu mahakamani kwa takribani miaka 15.

Katika hatua mpya ya mgogoro huo, wananchi hao wakiongozwa na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sokoni One, Michael Kivuyo, wanadai walikubaliana kulipwa Sh milioni 10 kila mmoja, sawa na Sh milioni 80, pamoja na kupewa maeneo kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza mgogoro huo.

Hata hivyo, Kivuyo amesema hadi sasa ni Sh milioni 40 pekee zilizotolewa na kugawanywa kwa baadhi ya wananchi, huku wengine wakidai kusubiri malipo yao kwa takribani mwaka mmoja.

Kivuyo, ambaye pia ametajwa kuwa miongoni mwa wananchi wanane waliosaini na kupokea Sh milioni 10, yeye  binafsi amekana kuchukua, amesema awali walielezwa kuwa kila mmoja angelipwa kiasi hicho, lakini baadaye fedha zilizopatikana hazikufikia kiasi kilichokubaliwa kwa kundi lote.

“Walikuwa wamekubali kulipa Sh milioni 10 kwa kila mmoja. Lakini baadaye walitoa Sh milioni 40 wakati tuko watu wanane. Kwa hiyo tukagawana, lakini wengine tuliambiwa tutapata, tusubiri,” amesema Kivuyo.

EKARI MOJA YAZUA MASWALI

Mbali na fedha hizo, Kivuyo amesema wananchi hao walikabidhiwa eneo la ekari moja, lakini hadi sasa hawajaruhusiwa kuliendeleza licha ya eneo hilo kuwa sehemu ya makubaliano ya kumaliza mgogoro.

Amesema hali hiyo imeendelea kuwa chanzo cha malalamiko kwa kuwa wananchi hao wanaamini walikabidhiwa eneo hilo kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano, lakini hawana uhuru wa kulitumia kwa shughuli za maendeleo.

“Eneo lenyewe tumekabidhiwa, lakini hadi sasa hatujaruhusiwa kuliendeleza. Ndiyo maana bado tunasema kuna tatizo ambalo linahitaji kufafanuliwa,” amesema.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Kivuyo na Diwani mstaafu wa Jiji la Arusha, Isaya Doita, katika makubaliano ya kumaliza mgogoro huo kulikuwa na suala la ekari tano ambazo Kituo cha Huruma kilikubali kuziachia kutoka katika eneo la ekari 15 lililokuwa kwenye mgogoro.

Inaelezwa kuwa wananchi walitakiwa kupata maeneo hayo kwa utaratibu uliokubaliwa, huku Halmashauri ikieleza pia kuhusu kuwapatia viwanja vingine na kubaki na sehemu ya eneo hilo.

‘SH MILIONI 40 ZILITOKA WAPI?’

Suala la chanzo na utaratibu wa malipo ya Sh milioni 40 limeibua maswali mapya.

Kivuyo amesema fedha hizo ziliwasilishwa katika mchakato uliomhusisha mwanasheria wa Jiji la Arusha, lakini nyaraka walizosaini wakati wa kupokea fedha hizo zilionyesha kuwa fedha hizo zilitoka katika kampuni binafsi iliyopo jijini Arusha.

“Sh milioni 40 walioletwa, sisi tulisaini kupitia mwanasheria ambaye alikuwa mwakilishi wa Jiji hapa mjini. Lakini kwenye nyaraka tulizosaini, inaonekana kama zinatoka kwenye kampuni binafsi,” amesema.

Amesema hali hiyo imewafanya kutaka kujua uhusiano wa kampuni hiyo na Halmashauri, mamlaka iliyoiwezesha kutoa fedha hizo na sababu ya fedha hizo kutotolewa moja kwa moja na Halmashauri iwapo ndiyo iliyokuwa na jukumu la kutekeleza makubaliano.

DIWANI MSTAAFU AHOJI UTARATIBU

Akizungumzia mgogoro huo, Doita amesema suala hilo linahitaji ufafanuzi wa kina, akitaka kujulikana nani aliidhinisha malipo ya Sh milioni 40, fedha hizo zilitoka wapi na zilitolewa kwa mamlaka gani.

Doita amesema kabla ya Baraza la Madiwani kuvunjwa, kulikuwa na makubaliano ya kumaliza mgogoro huo nje ya mahakama baada ya Halmashauri kuwaomba wananchi hao kuondoa kesi ili suala hilo limaliwe kwa maelewano.

Amesema kwa mujibu wa makubaliano hayo, Halmashauri ilikubali kuwafidia wananchi hao gharama walizotumia katika uendeshaji wa kesi, kiasi cha Sh milioni 10 kwa kila mmoja, huku Kituo cha Huruma kikikubali kuachia sehemu ya eneo lililokuwa kwenye mgogoro.

“Kinachonishangaza ni kwamba kama Halmashauri ndiyo iliyokuwa na jukumu la kuwalipa wananchi hao, kampuni au mtu binafsi ameingiaje katika suala hili? Nani alikubaliana naye na kwa utaratibu gani?” amehoji Doita.

Doita, ambaye amewahi kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali za Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwamo Kamati ya Fedha, amesema wakati suala hilo likijadiliwa waliridhia kwa kuzingatia kuwa wananchi hao walikuwa wametumia muda na fedha nyingi katika kesi hiyo.

“Tuliridhia kama Kamati ya Fedha kwa sababu watu hawa walitumia gharama na muda wao mwingi katika kesi. Lakini cha kushangaza sasa ni kwamba kama Halmashauri ndiyo ilikuwa responsible kuwalipa, wamewalipa nani na kwa utaratibu gani?” amehoji.

‘MALI YA HALMASHAURI NI MALI YA UMMA’

Doita amesema jambo jingine linalopaswa kuwekwa wazi ni hatima ya eneo lililokubaliwa kutolewa kwa wananchi hao, likiwamo kujulikana kama limepimwa, lilipo na kama bado liko chini ya Halmashauri au limehamishiwa kwa mtu mwingine.

“Mali ya Halmashauri ni mali ya umma. Tunataka utaratibu uzingatiwe, tunataka sheria zizingatiwe na tunataka tujue mali hii iko wapi na inaendelea kutumikaje,” amesema.

Amesema iwapo kampuni au mtu binafsi alihusika kutoa fedha kwa wananchi hao kwa niaba ya Halmashauri, ni muhimu mamlaka husika kueleza msingi wa uamuzi huo.

Kwa maelezo yake, matumizi au uhamishaji wa mali ya Halmashauri unapaswa kufuata taratibu za kisheria na kiutawala, ikiwamo kupitia vyombo husika vya maamuzi vya Halmashauri, Kamati ya Fedha na Baraza la Madiwani.

“Huwezi kuchukua mali ya umma na kuifanya mali ya mtu bila utaratibu. Kamati husika inapaswa kukaa, Baraza liketi na kuwe na uamuzi wa pamoja. Hii ndiyo njia ya kulinda mali ya umma,” amesema.

SARUN: ‘MIMI PIA SIKUPATA’

Kwa upande wake, Diwani mstaafu wa Sokoni One, Sarun Olodi, amesema suala hilo lipo katika mchakato wa kushughulikiwa na mamlaka aliyoikataa kuitaja, akiahidi kulizungumzia kwa kina baada ya wiki mbili.

Sarun amesema yeye ni miongoni mwa wananchi ambao hawakupokea fedha hizo na kwamba wamekuwa wakizungushwa bila kujua wanapaswa kudai kwa nani.

Amesema anajiandaa kuzungumza na waandishi wa habari na kuweka hadharani taarifa zote anazodai kuwa amekuwa akizifahamu kuhusu suala hilo.

“Mimi ni miongoni mwa wananchi ambao hawakupokea kiasi hicho cha fedha. Tumekuwa tukizungushwa, hatujui tunadai nani. Jambo hili lilikuwa siri, lakini sasa nitalizungumza hadharani ili tupate fedha tulizoahidiwa na hatimaye tuweze kuondoa kesi mahakamani,” amesema Sarun.

Amesema anatarajia kuzungumza na vyombo vya habari wiki ijayo na kutoa maelezo zaidi kuhusu mgogoro huo.

MASWALI BADO YANASUBIRI MAJIBU

Kwa sasa, mgogoro huo umeacha maswali kadhaa yanayohitaji majibu kutoka kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha na wahusika wengine.

Maswali hayo ni pamoja na: Nani alilipa Sh milioni 40? Fedha hizo zilitolewa kwa mamlaka gani? Kwa niaba ya nani? Kwa nini Halmashauri haikulipa moja kwa moja? Kwa nini wananchi wanne bado hawajalipwa Sh milioni 10 kila mmoja? Na hatima ya ekari tano zilizokuwa sehemu ya makubaliano ni ipi?

Aidha, bado kuna swali la msingi kuhusu eneo la ekari moja ambalo wananchi wanasema walikabidhiwa lakini hawajaruhusiwa kuliendeleza.

Doita amesema ni muhimu mamlaka husika kutoa taarifa kamili kuhusu fedha hizo, nyaraka walizosaini wananchi, eneo lililotolewa na utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa ili kuondoa sintofahamu.

Kwa upande wake, Kivuyo amesema wananchi wanataka kila kilichokubaliwa kiwekwe wazi na kitekelezwe kwa usawa kwa wananchi wote wanane.

“Wataita nyote, tutazungumza. Dunia ijue kwamba nini kinaendelea pale,” amesema.

Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, ili kutoa ufafanuzi kuhusu madai hayo zinaendelea.

Mgogoro huo, ambao ulianza katika eneo la ekari 15 na kudumu mahakamani kwa takribani miaka 15, sasa umeingia katika sura mpya huku Sh milioni 40, madai ya Sh milioni 80, ekari moja iliyokabidhiwa bila kuruhusiwa kuendelezwa na utata wa ekari tano vikiwa kiini cha maswali mapya yanayoendelea kutaka majibu.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم