MAVUNDE ATOA WIKI MOJA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA WA TANZANITE
Na Joseph Ngilisho | MERERANI
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa wiki moja kwa Kamishna wa Madini na timu yake kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wachimbaji wa Tanzanite Mirerani, akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya madini hayo nchini.
Mavunde alitoa agizo hilo Agosti 24,2026 wakati wa ziara yake katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, ambapo alitaka wataalamu wa Serikali kutembelea vituo vya kuongeza thamani ya madini, ikiwemo kituo cha gemolojia cha TGC kilichopo Arusha, ili kujifunza namna bora ya kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara wa Tanzanite.
Alisema wataalamu hao wanapaswa kwenda na timu yao yote katika kituo hicho ili kujifunza na kuona namna ambavyo huduma za kuongeza thamani zinaweza kuimarishwa na kuwasaidia wananchi wanaojihusisha na biashara ya madini.
“Waende wote wakajifunze pale, waone namna nzuri ya kuweza kusaidia kuongeza thamani. Kamishna, naelekeza iwe ndani ya wiki hii. Tiketi iandaliwe vizuri, kisha siku yote kabla ya Ijumaa mambo haya yaende kufanyika pale,” alisema Mavunde.
Alisema endapo kutakuwa na changamoto nyingine zinazozuia wananchi kunufaika na shughuli za madini, Serikali inapaswa kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji na biashara zinaendelea kuwa na tija kwa wananchi na Taifa.
WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUHAMIA ENEO MOJA
Katika hatua nyingine, Mavunde alisisitiza umuhimu wa kuwaweka pamoja wafanyabiashara wa madini katika eneo rasmi la biashara, akisema hatua hiyo itarahisisha Serikali kufanya ufuatiliaji na kudhibiti shughuli za biashara ya madini.
Alisema shughuli nyingi za Mirerani zinahusiana moja kwa moja na madini, hivyo kuwepo kwa mfumo mzuri wa uendeshaji wa biashara ya madini kutasaidia kuongeza tija katika eneo hilo.
“Kwa sababu utumishi hapa Mirerani kwa asilimia kubwa sana ni wa madini. Hata mfumo wa uendeshaji uwe ndani na shughuli kuu ya hapa ni madini. Kwa mimi kuna tija kubwa sana,” alisema.
Mavunde alisema wafanyabiashara wa Tanzanite wanaofanya biashara katika maeneo mbalimbali ya mji wanapaswa kuhamishiwa katika eneo maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema hatua hiyo itarahisisha ufuatiliaji wa biashara, kuongeza usalama na kuwezesha Serikali kupata taarifa sahihi kuhusu biashara ya madini inayofanyika Mirerani.
BILIONI 9 KUKAMILISHA JENGO
Kuhusu jengo la kituo cha biashara ya madini Mirerani, Mavunde alisema Serikali inaendelea na dhamira ya kulikamilisha, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono ujenzi wa jengo hilo.
Alisema zaidi ya Sh bilioni tisa zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, huku akisisitiza kuwa litakapokamilika linapaswa kutumika kikamilifu katika kuimarisha biashara ya madini Mirerani.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati ya ujenzi wa hili jengo. Ilikuwa ni ahadi yake, imetimia. Zaidi ya Sh bilioni tisa zitakuwa kuwepo hapa kukamilisha ujenzi wa jengo hili,” alisema.
Alisema Wizara ya Madini itashirikiana na wizara na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha changamoto zilizobaki zinatatuliwa ili ujenzi ukamilike kwa wakati na shughuli za biashara ya madini ziweze kufanyika katika mazingira rasmi na salama.
Mavunde alisema umuhimu wa kukamilisha miundombinu hiyo unatokana na nafasi kubwa ya madini katika uchumi wa Mirerani na Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha wananchi wanaopatikana katika mnyororo mzima wa thamani wa Tanzanite wananufaika zaidi na rasilimali hiyo.


إرسال تعليق