SERIKALI KULIFANYIA UTAFITI ENEO LA TANZANITE MERERANI
Na Joseph Ngilisho | MERERANI
Uamuzi huo umetangazwa Agosti 24,2026 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati wa ziara maalum ya kukagua mfumo mzima wa uchimbaji, uzalishaji na biashara ya Tanzanite Mererani, akisema Serikali itaelekeza nguvu zaidi katika utafiti wa kisayansi ili wachimbaji wasiendelee kutumia fedha nyingi kuchimba maeneo yasiyo na uhakika wa kupata madini.
Mavunde alisema Serikali itatumia mpango wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya sekta ya madini kwa ajili ya utafiti, ambapo Mererani itapewa kipaumbele kutokana na umuhimu wa Tanzanite kwa uchumi na utambulisho wa Tanzania duniani.
Alisema kwa muda mrefu wachimbaji wamekuwa wakielekeza shughuli zao katika maeneo yanayozunguka Kitalu C kwa imani kuwa ndiko pekee kuna uwezekano mkubwa wa kupata Tanzanite, hali ambayo imeongeza gharama za uchimbaji na kuchangia changamoto za mitobo ya migodi.
Kwa mujibu wa Mavunde, Serikali sasa inataka kuachana na mfumo wa uchimbaji wa kubahatisha na badala yake kutumia teknolojia na tafiti za kitaalamu kubaini maeneo yenye uwezekano wa kuwa na madini hayo.
Alisema amemwelekeza Kamishna wa Madini kurejea Mererani na kukutana na wataalamu wa jiolojia kutoka kampuni zinazochimba Tanzanite, akiwemo Franone na Chusa, ili kuandaa mfumo bora wa kufanya utafiti wa maeneo mapya.
“Kaeni wote, mtuambie mfumo mzuri wa kufanya utafiti pale ni upi ili katika mpango wetu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya sekta ya madini, Mererani ipewe kipaumbele na tuongeze eneo kubwa zaidi la utafiti,” alisema.
Wakati Serikali ikipanga kupanua utafiti, Mavunde alisema pia imeanza mchakato wa kubadili mfumo wa biashara ya Tanzanite, kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wazawa wanapata nafasi na manufaa makubwa zaidi kutokana na rasilimali hiyo.
Alisema Serikali imebaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wenye leseni ambao wamekuwa wakitumia nafasi zao kuingiza wageni katika biashara ya Tanzanite, jambo alilosema linaweza kusababisha nguvu ya kuamua bei kubaki mikononi mwa kundi dogo la watu.
“Tunakwenda kufanya operesheni maalum. Kama kuna mtu ana utaratibu wa kuingiza watu kwa mgongo huo, tutakwenda kukaa na Waziri wa Kazi na Ajira, tutengeneze mfumo pamoja ili kukabiliana na changamoto ya kutengeneza ‘cartel’ kwenye madini yetu ya Tanzanite,” alisema.
Alisema Serikali inalenga kujenga ushindani wa kweli katika biashara hiyo ili kuzuia hali ya bei ya Tanzanite kuamuliwa na kundi dogo la wafanyabiashara.
Mavunde alisema miongoni mwa mapendekezo yanayoweza kujadiliwa ni kuweka mfumo wa kati wa kusimamia ununuzi na biashara ya Tanzanite, kwa lengo la kuongeza uwazi na kuimarisha nguvu ya wazalishaji katika soko.
FRANONE, CHUSA WAAGIZWA
Maelekezo kama hayo yalitolewa kwa wachimbaji wa Chusa na wamiliki wa leseni nyingine, akiwataka kuandaa mipango ya muda mfupi na mrefu itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa Tanzanite.
Mavunde alisema ziara yake Mererani imetokana na maombi ya Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, Chama cha Brokers Tanzania na wadau wengine wa sekta ya madini, lakini pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu maboresho ya mfumo wa uchimbaji na biashara ya Tanzanite.
Alisema timu iliyoundwa mwaka 2023 kuchunguza mfumo wa uchimbaji na biashara ya Tanzanite tayari imekamilisha kazi yake na kutoa mapendekezo, huku Serikali ikiwa katika hatua ya kuyafanyia kazi na kuyaweka katika utekelezaji.
“Nimekuja hapa kwa ajili ya kutimiza maombi hayo yote, lakini kubwa kuliko yote ni maelekezo ya Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Waziri huyo alikagua mgodi wa Franone, mgodi wa Chusa, Soko la OPEC na eneo la tathmini ya madini, akisema ziara hiyo imempa picha pana ya hali halisi ya uchimbaji na biashara ya Tanzanite.
Alisema baadhi ya hatua zitakazochukuliwa zinaweza kutowafurahisha baadhi ya wadau mwanzoni, lakini zitakuwa na lengo la kutibu changamoto zilizopo.
“Korokwini ni chungu, lakini inatibu. Mapendekezo yanaweza yasifurahishe sana katika hatua za awali, lakini ndiyo njia pekee ya kutibu changamoto hii,” alisema.
OLE MILLYA: TANZANITE IBEBE BENDERA YA TANZANIA
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, ameitaka Serikali kuongeza nguvu katika utafiti, uchimbaji na biashara ya Tanzanite, akisema madini hayo ni sehemu ya utambulisho wa Tanzania na yanapaswa kuwa chanzo kikubwa cha manufaa kwa wananchi na Taifa.Ole Millya alisema Serikali inapaswa kuangalia mnyororo mzima wa thamani wa Tanzanite, kuanzia utafiti, uchimbaji, mitaji, ununuzi, uongezaji thamani hadi masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Kwa sababu tunajua jina la Tanzania, Mheshimiwa Waziri, ni vyema tukaangazia macho yetu na kubeba bendera ya nchi kwa madini haya,” alisema.
Alisema gharama za uchimbaji wa Tanzanite ni kubwa na baadhi ya wachimbaji wamewekeza kwa muda mrefu, hivyo maboresho ya mfumo wa sekta hiyo yanapaswa kuzingatia uwekezaji uliopo na kusikiliza maoni ya wachimbaji wadogo, wafanyabiashara, wanawake na wadau wengine.
Ole Millya alisema ujio wa Waziri Mererani ni ishara ya Serikali kusikiliza changamoto za wananchi na wadau wa sekta hiyo, akisisitiza kuwa lengo la mwisho linapaswa kuwa kuhakikisha wananchi wanapata manufaa kutokana na rasilimali iliyopo katika ardhi yao.
“Tumekabidhiwa dhamana ya kuwahudumia wananchi. Hii ndiyo maana ya Serikali; kusikiliza wananchi, kuelewa changamoto zao na kuhakikisha mwisho wa siku wanapata furaha na manufaa ya rasilimali zilizopo nchini,” alisema.
Alisema wananchi wa Simanjiro wako tayari kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa hatua zitakazochukuliwa kuboresha uchimbaji na biashara ya Tanzanite.
Aidha, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kulinda na kukuza sekta ya madini, hususan Tanzanite, ambayo imekuwa sehemu ya utambulisho wa Tanzania kimataifa.
Ziara hiyo imekuja wakati Serikali ikitafuta njia mpya za kuongeza uzalishaji, kudhibiti changamoto za biashara na kuhakikisha Tanzanite inazalisha thamani kubwa zaidi kwa wachimbaji, wafanyabiashara wazawa na Taifa kwa ujumla.
Ends











Post a Comment