Breaking🔥

TUME YA JAJI LILA YALENGA WALIYEPANGA, KUFADHILI NA KUTEKELEZA GHASIA

 TUME YA JAJI LILA YALENGA WALIYEPANGA, KUFADHILI NA KUTEKELEZA GHASIA

Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Tume ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, amesema tume hiyo ina mamlaka na jukumu tofauti na Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 24, 2026, Jaji Lila amesema tume iliyoongozwa na Jaji Chande ilijikita zaidi katika kuchunguza matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, pamoja na kubaini aina na kiwango cha vurugu na uvunjifu wa amani uliojitokeza.

Amesema tofauti na tume hiyo, Tume anayoiongoza imepewa jukumu la kwenda hatua zaidi kwa kubaini watu waliohusika katika kupanga, kuratibu, kufadhili na kutekeleza matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria.

“Jukumu letu ni kuchunguza na kubaini wahusika wa matukio hayo, wakiwemo waliopanga, waliyoratibu, waliofadhili na waliotekeleza,” amesema Jaji Lila.

Aidha, amesema tume itachunguza madhara yaliyosababishwa na ghasia hizo, ikiwemo kubaini watu waliojeruhiwa na waliopoteza maisha, pamoja na mazingira na wahusika waliohusika katika kusababisha madhara hayo.

Jaji Lila amesema tume hiyo pia itachunguza aina na kiwango cha nguvu kilichotumika na vyombo vya dola katika kudhibiti ghasia, ili kubaini iwapo hatua zilizochukuliwa zilizingatia sheria, taratibu na viwango vinavyotakiwa.

Tume hiyo, inayojulikana kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa rasmi Agosti 7, 2026.

Inaundwa na majaji wastaafu pamoja na majaji kutoka nje ya Tanzania, ikiwa na jukumu la kuchunguza kwa kina wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Jaji Lila amesema uchunguzi huo unalenga kuweka wazi ukweli kuhusu matukio hayo, wahusika wake, madhara yaliyotokea na namna nguvu ilivyotumika katika kuyadhibiti.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post