Breaking🔥

BASI LA MIZA EXPRESS LAUA WANNE NZEGA WAMO WATOTO

WATU WANNE, WAKIWEMO WATOTO WAWILI, WAFARIKI AJALI YA MIZA EXPRESS NZEGA

Na Joseph Ngilisho | NZEGA

WATU wanne, wakiwemo watoto wawili, wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Miza Express lililokuwa likitoka Mpanda kwenda Bariadi kupata ajali katika eneo la Kijiji cha Ngukumo, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa 9:20 usiku, baada ya basi hilo kuacha njia, kugonga vyuma vya kingo za barabara na kisha kupinduka na kutumbukia bondeni, kilomita chache kabla ya kufika makao makuu ya Wilaya ya Nzega.

Baadhi ya abiria walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya matibabu, huku abiria wengine walionaswa ndani ya basi hilo wakilazimika kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Twawa Juma Lulengelule, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema watu wanne wamefariki, wakiwemo wanaume watatu na mwanamke mmoja.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa ajali hiyo imesababishwa na dereva kukosa umakini na kushindwa kulimudu basi hilo, lililoacha njia na kugonga vyuma vya kingo za barabara kabla ya kupinduka na kutumbukia bondeni.

Kamanda Lulengelule amesema uchunguzi zaidi unaendelea kubaini kwa kina mazingira ya ajali hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post