Breaking🔥

LISHE YA BAHARINI YATAJWA KUWA SIRI YA KUJENGA AKILI ZA WATOTO, WAZAZI WATAKIWA KUITUMIA VYEMA.

 LISHE YA BAHARINI YATAJWA KUWA SIRI YA KUJENGA AKILI ZA WATOTO, WAZAZI WATAKIWA KUITUMIA VYEMA. 

Na Hadija Bagasha Tanga, 

WAZAZI wanaoishi katika ukanda wa pwani wametakiwa kutumia ipasavyo fursa ya upatikanaji wa vyakula vya baharini kwa kuwapatia watoto wao lishe bora, baada ya kubainishwa kuwa vyakula hivyo vina mchango mkubwa katika ukuaji wa ubongo, kuongeza uwezo wa kufikiri na kuwasaidia watoto kufanya vizuri zaidi katika masomo yao wawapo mashuleni. 


Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Centre for Education Yusuf Ugutu, alipokuwa akizungumza na wazazi wa wanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Mwapachu iliyopo Jijini Tanga.


Ugutu alisema jamii za ukanda wa pwani zimebarikiwa kuwa karibu na rasilimali za bahari zenye vyakula vyenye virutubisho muhimu vinavyochangia ukuaji wa ubongo wa mtoto, jambo linaloongeza uwezo wa kuelewa, kujifunza kwa haraka na kufanya vizuri darasani.

Alisisitiza kuwa vyakula vya baharini vinavyopatikana kwa wingi katika ukanda wa pwani ni fursa ambayo wazazi wanapaswa kuitumia kwa manufaa ya watoto wao, kwani vina mchango mkubwa katika kujenga afya ya ubongo na kuongeza uwezo wa watoto kujifunza.

Alisema wazazi hawapaswi kuwa na hofu kwamba watoto wao hawana akili au uwezo mdogo wa kujifunza, akieleza kuwa mara nyingi tofauti hujitokeza katika namna watoto wanavyotumia maarifa waliyonayo pamoja na mazingira wanayolelewa.

"Mzazi asione mtoto wake hana akili Kila mtoto ana uwezo wake Tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha anapata lishe bora, malezi mazuri na mazingira yanayomwezesha kutumia uwezo wake ipasavyo," alisema Ugutu.

Aidha, aliwahimiza wazazi kusimamia kwa karibu lishe ya watoto wao pamoja na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma, akieleza kuwa ushirikiano kati ya familia na shule ni msingi muhimu wa kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Ugutu alisema endapo wazazi watazingatia lishe bora, kuwajengea watoto mazingira mazuri ya kujifunza na kuendelea kuwapa motisha, wataongeza nafasi ya watoto wao kufanya vizuri katika masomo na kufikia ndoto zao za kielimu.

Katika hatua nyingine Ugutu amewataka wazazi kuhakikisha wanawasimamia watoto wao kwa ukaribu zaidi ili kuona matokeo wanayoyapata ikiwa ni pamoja na kukagua masomo yao ya kila siku ili kumjenga mwanafunzi kuwa makini. 

"Wazazi wote, sisi wadau wa elimu, na walimu kuhakikisha tunashirikiana kwa pamoja ili ufaulu wa watoto wetu uwe mzuri ili wawe bora zaidi sisi Tanga yetu tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi za elimu katika jiji la Tanga, "alisisitiza Ugutu. 

Baadhi ya wazazi wameiomba Serikali kuwapatia taarifa mapema panapokuwepo na mabadiliko ya mitaala mipya kwenda ujio wa mitaala mipya kwa kipindi kifupi unakwenda kuwaathiri wanafunzi kwenye mitihani yao kwani wanakuwa hawajajiandaa ipasavyo. 

"Kama kuna mitaala mipya serikali tunaishauri serikali iseme mapema ili watoto waweze kujiandaa kwa mfano kama mtaala ni mpya basi ianze januari ili watoto wajiandae vizuri, "alisema mmoja wa wazazi hao. 

Mwisho.

Post a Comment

أحدث أقدم