ARUMERU YAPOKEA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM, SH BILIONI 24 ZATUMIKA
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru kimepokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, ikieleza utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh bilioni 24 zilizotolewa na Serikali katika kipindi cha miezi sita, kuanzia Januari hadi Juni 2026.Taarifa hiyo imesomwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Mwinyi,Agosri 282026 katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru, ambapo alieleza hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Katika sekta ya ajira, amesema jumla ya watumishi 123 wameajiriwa katika kada mbalimbali, zikiwemo elimu, afya, fedha, manunuzi, mipango na uratibu, utawala, miundombinu, TEHAMA, maliasili, sheria, kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha, amesema jumla ya ajira za muda 1,407 zimepatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo ya halmashauri hiyo.
ELIMU YA BURE
Akizungumzia elimu, Mwinyi amesema Halmashauri ya Arumeru imeendelea kutekeleza mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi na sekondari, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesema katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026, sekta ya elimu sekondari ilipokea Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, fedha zilizotumika kugharamia mahitaji mbalimbali ya shule, ikiwemo uendeshaji wa ofisi, chakula cha wanafunzi, mabweni na posho za madaraka kwa wakuu wa shule.
Mwinyi amesema halmashauri inasimamia jumla ya shule 179, zikiwemo shule za Serikali na binafsi.
Amesema katika mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2026, jumla ya wanafunzi 958 walifanya mtihani huo na kufanikiwa kupata ufaulu wa asilimia 100.
Katika elimu ya awali na msingi, amesema jumla ya wanafunzi 11,831 wameandikishwa darasa la awali, wakiwemo wavulana 6,044 na wasichana 5,787.
ARUMERU YANG'ARA MICHEZONI
Katika sekta ya michezo, Mwinyi amesema halmashauri imeendelea kuratibu ushiriki wa wanafunzi katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kuanzia ngazi ya shule hadi taifa.
Amesema Arumeru imefanikiwa kupata makombe nane na medali sita, huku wanafunzi wanne wakichaguliwa kujiunga na timu ya Mkoa wa Arusha iliyoshiriki mashindano ya kitaifa.
Pia amesema halmashauri imefanikiwa kuendesha mabonanza nane pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya michezo.
AFYA
Katika sekta ya afya, Mkuu huyo wa Wilaya amesema halmashauri imeendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Amesema shughuli nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na udhibiti wa malaria, chanjo, upimaji wa hiari na huduma nyingine za afya.
Kuhusu miundombinu, amesema Serikali Kuu imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya kuboresha Hospitali ya Wilaya pamoja na kujenga na kuboresha vituo vya afya, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mwinyi amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa na wananchi wanapata huduma bora za kijamii na kiuchumi.
Mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru umeendelea na mjadala wa utekelezaji wa Ilani pamoja na tathmini ya shughuli za maendeleo zinazotekelezwa katika wilaya hiyo.
Ends..


Post a Comment