Breaking🔥

CCM ARUMERU YAMPONGEZA RAIS SAMIA KUMTEUA NDEJEMBI MAKAMU WA RAIS,SEVERE ASEMA TAIFA LIMELAMBA DUME

CCM ARUMERU YAMPONGEZA RAIS SAMIA KUMTEUA NDEJEMBI MAKAMU WA RAIS

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua Deogratias Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikisema uteuzi huo ni ishara ya imani kwa vijana katika uongozi wa nchi.

Pongezi hizo zimetolewa leo Ijumaa Agosti 28,2026 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe, wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru uliokuwa ukipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Severe alisema CCM Arumeru imefurahishwa na uteuzi huo na inaunga mkono kwa asilimia 100, akieleza kuwa uamuzi wa viongozi wa juu wa chama kumteua Ndejembi ulikuwa wa busara na sahihi.

“CCM Wilaya ya Arumeru tuko nyuma yao, tunawaunga mkono na tumefurahishwa sana. Tunaamini maamuzi yale yalikuwa ya busara. Kumchagua ndugu yetu Deogratias Ndejembi hawajakosea, wako sahihi, na sisi tuko nyuma yao kwa asilimia 100,” alisema Severe.


Aidha, Severe aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Arumeru, akisema CCM imekuwa ikifuatilia na kukagua utekelezaji wa Ilani katika maeneo mbalimbali.

Alisema ndani ya kipindi cha miezi sita, Serikali imeendelea kuleta miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 24 wilayani humo.

“Tumefuatilia utekelezaji wa Ilani, tumekagua na ndani ya miezi sita Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuneemesha kwa miradi ya Sh milioni 24 na zaidi. Nani kama Mama Samia?” alisema.

Severe pia aliwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Meru, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri, Baraka, pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, kwa mchango wao katika kusimamia utekelezaji wa Ilani na maendeleo ya wananchi.

Pamoja na hayo, aliwapongeza Mkurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa idara na taasisi mbalimbali kwa kazi wanayoifanya katika kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa na wananchi wanapata huduma zinazostahili.

Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi wa CCM kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na upendo, akisema misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha chama kinaendelea kuwaunganisha viongozi na wananchi katika kusimamia maendeleo.

“CCM tumechagua umoja, mshikamano na upendo kuhakikisha kazi zinafanyika na kuhudumia wananchi wetu. Tuendelee hivyo hivyo kwa mshikamano pamoja na kufanya kazi kwa umoja wa kweli,” alisema.

Aidha, Severe aliwapongeza wenyeviti wa kata, makatibu, wanenezi na viongozi wengine wa CCM kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani katika kata zao, pamoja na madiwani kwa kazi wanayoifanya kwa mshikamano.

Aliwataka viongozi hao kuendelea kushirikiana na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM unaendelea kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi wa Arumeru.

Post a Comment

Previous Post Next Post