WATUHUMI 21 WAKAMATWA LONGIDO, WAKITOROSHA MIFUGO 1,955 KWA MAGENDO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WATUHUMIWA 21 wamekamatwa katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji haramu wa mifugo kwenda nchi jirani kwa njia za magendo, huku jumla ya mifugo 1,955 ikikamatwa kabla ya kuvushwa nje ya Tanzania.
Hatua hiyo imechukuliwa na Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) kwa kushirikiana na Maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kupitia doria za pamoja zinazolenga kudhibiti wizi wa mifugo pamoja na usafirishaji wa mifugo nje ya nchi bila vibali.
Akizungumza leo, Agosti 26, 2026, Kamanda wa STPU, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika kipindi cha kuanzia Juni 2026 hadi sasa, wakati wakijaribu kusafirisha mifugo hiyo kwenda nchi jirani bila kufuata taratibu na kupata vibali vinavyotakiwa.
SACP Pasua amesema operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kudhibiti vitendo vya wizi na biashara haramu ya mifugo, hususan katika maeneo ya mipakani ambako baadhi ya watu wamekuwa wakitumia njia zisizo rasmi kuvusha mifugo kwenda nchi jirani.
Amesema doria hizo za pamoja zimeendelea kuimarishwa katika maeneo yanayotajwa kuwa na changamoto ya usafirishaji haramu wa mifugo, huku vyombo vya dola na wataalamu wa mifugo wakishirikiana kuhakikisha mifugo inayosafirishwa inafuata sheria na taratibu zilizowekwa.
WATUHUMIWA 42 WAKAMATWA KWA WIZI
Mbali na kukamatwa kwa watuhumiwa 21 waliokuwa wakitorosha mifugo, SACP Pasua amesema katika kipindi hicho jumla ya watuhumiwa 42 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na wizi wa mifugo.
Amesema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, huku mmoja wao akiwa tayari amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, wakati kesi za watuhumiwa wengine zikiendelea katika hatua mbalimbali za kisheria.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, hatua hizo zinaonyesha namna kikosi hicho kinavyoendelea kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya wizi wa mifugo, ambao umekuwa ukiathiri maisha na uchumi wa wafugaji pamoja na kuchochea migogoro katika baadhi ya maeneo.
ELIMU KWA JAMII YAONGEZWA
SACP Pasua amesema STPU haitumii nguvu za kisheria pekee katika kukabiliana na uhalifu wa mifugo, bali imekuwa ikiweka mkazo katika ushirikishwaji wa wananchi na utoaji wa elimu kuhusu namna ya kuzuia uhalifu kabla haujatokea.
Amesema katika kipindi hicho kikosi kimefanya jumla ya mikutano 305 ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikutano inayofanyika katika maeneo ya minada ya mifugo.
Amesema mikutano hiyo inalenga kuwaelimisha wafugaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kulinda mifugo, kutoa taarifa za uhalifu na kuhakikisha shughuli za uuzaji na usafirishaji wa mifugo zinafanyika kwa kuzingatia sheria.
“Lengo letu ni kujenga miundombinu ya amani mapema kabla ya uhalifu haujatokea,” amesema SACP Pasua.
Amesema ushirikishwaji wa jamii ni nguzo muhimu katika kupambana na wizi wa mifugo, kwa kuwa wananchi wana nafasi kubwa ya kubaini viashiria vya uhalifu na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kabla ya madhara makubwa kutokea.
Amehimiza wafugaji na wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika na mifugo, akisisitiza kuwa taarifa za haraka kutoka kwa jamii zinaweza kusaidia kuzuia wizi, kukamatwa kwa wahusika na kurejeshwa kwa mifugo inayopotea.
Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa mifugo, hususan katika maeneo ya mipakani, kwa lengo la kuhakikisha biashara ya mifugo inafanyika kwa mujibu wa sheria na kuzuia wizi pamoja na utoroshaji wa mifugo nje ya nchi.

Post a Comment