WANANDOA WALIOSUBIRI MTOTO KWA MIAKA 17 WAFANIKIWA KUPATA MTOTO ST. JOSEPH HOSPITAL ARUSHA.

 WANANDOA WALIOSUBIRI MTOTO KWA MIAKA 17 WAFANIKIWA KUPATA MTOTO ST. JOSEPH HOSPITAL ARUSHA.

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

ARUSHA – Furaha na shangwe zimeikumba familia moja kutoka Mkoa wa Tabora baada ya ndoto yao ya kupata mtoto kutimia kufuatia miaka mingi ya kusubiri, baada ya kupata huduma za kibingwa katika Hospitali ya St. Joseph.

Wanandoa hao, waliokuwa wakisubiri kupata mtoto tangu walipofunga ndoa mwaka 2009, wamefanikiwa kujifungua salama mtoto wa kiume kupitia huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo, hatua iliyorejesha matumaini kwa familia hiyo iliyokuwa imepitia safari ndefu ya kutafuta tiba.

Akizungumza hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Uzazi na Umauzazi wa Kina Mama, Dkt. Mgeta, alisema wanandoa hao walifika St. Joseph Hospital takribani wiki mbili zilizopita wakiwa na historia ya changamoto za uzazi kwa muda mrefu.

Alisema baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu kwa kutumia vifaa na teknolojia ya kisasa pamoja na huduma za kibingwa zinazopatikana hospitalini hapo, walifanikiwa kupata mtoto wa kiume akiwa na afya njema.

"Ni jambo la faraja kuona familia iliyokuwa imekata tamaa kwa miaka mingi leo inatabasamu baada ya kupata mtoto. Haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika huduma za kibingwa, vifaa vya kisasa na wataalamu wenye uzoefu ambao Hospitali ya St. Joseph imeendelea kuuweka kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania," alisema Dkt. Mgeta.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanaendelea kuthibitisha nafasi ya Hospitali ya St. Joseph kama moja ya vituo vinavyoongoza nchini katika utoaji wa huduma za kibingwa za afya ya uzazi na mama na mtoto, huku ikipokea wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali wanaotafuta tiba za kisasa na zenye matokeo chanya.

Dkt. Mgeta pia alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya St. Joseph, Joseph Mrosu, kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, vifaa tiba na kuboresha huduma za kibingwa, jambo linaloiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake, baba wa mtoto huyo, Naftali Sanga, mkazi wa Mkoa wa Tabora, alisema yeye na mke wake wamepitia safari ngumu ya kutafuta mtoto kwa zaidi ya miaka 15 bila mafanikio.

Alisema baada ya kufika Hospitali ya St. Joseph na kupatiwa huduma za kitaalamu kwa kipindi cha takribani wiki mbili, ndoto yao ya muda mrefu hatimaye imetimia kwa kumpata mtoto wa kiume.

"Tulikuwa tumekata tamaa baada ya miaka mingi ya kusubiri, lakini leo Mungu ametujalia kupitia mikono ya madaktari wa Hospitali ya St. Joseph. Hatuwezi kueleza furaha tuliyonayo. Tunawashukuru madaktari wote, hususan Dkt. Mgeta na uongozi wa hospitali kwa huduma bora, upendo na weledi waliotuonesha," alisema Sanga.

Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha sifa ya Hospitali ya St. Joseph kama kituo kinachotoa huduma za kibingwa zenye ubora wa hali ya juu, huku kikitoa matumaini mapya kwa familia nyingi zinazokabiliwa na changamoto za uzazi nchini.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post