VITA YA ARDHI YAFUKUTA MONDULI: WANANCHI WAMTUPIA DIWANI TUHUMA NZITO ZA KUPORA ENEO LA MALISHO, MBUNGE AAGIZA HATUA

 VITA YA ARDHI YAFUKUTA MONDULI: WANANCHI WAMTUPIA DIWANI TUHUMA NZITO ZA KUPORA ENEO LA MALISHO, MBUNGE AAGIZA HATUA

Na Arushadigital | MONDULI

MGOGORO wa ardhi umeibuka upya katika Kata ya Sepeko, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, baada ya wananchi kuibua tuhuma nzito dhidi ya Diwani wa kata hiyo, Kimai Diwani, wakimtuhumu kuhusika na kujimilikisha sehemu ya eneo la malisho la kijiji cha Alkaria kinyume cha utaratibu, madai ambayo yeye ameyakanusha akiyaita ya kisiasa.


Malalamiko hayo yaliibuliwa hadharani katika mkutano wa wananchi uliofanyika eneo la Mti Mmoja wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph, ya kukagua miradi ya maendeleo, kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili.

Wananchi walieleza kuwa migogoro ya ardhi imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha sintofahamu katika kata hiyo, wakidai baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa na madiwani wamekuwa wakihusika katika uporaji wa maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya jamii, hususan malisho ya mifugo.

Mmoja wa wananchi, Easter Ndani, alisema eneo la malisho la Eluwai, ambalo ni muhimu kwa wafugaji wa kijiji cha Alkaria, limevamiwa na kuchukuliwa kinyume cha sheria. Alidai kuwa pamoja na kuwepo kwa mipaka iliyowekwa na Serikali, baadhi ya alama za mipaka (bikoni) ziliondolewa, jambo lililochochea kuibuka kwa mgogoro huo.

"Tunategemea eneo hili kwa ajili ya mifugo yetu. Hatuwezi kuelewa kwa nini eneo la jamii lichukuliwe na mtu mmoja. Tunaomba Serikali iturejeshee haki yetu," alisema mwananchi huyo na kuonheza

“Tunamuomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie kurudisha eneo letu la LWI ambalo linachukuliwa kwa nguvu. Hilo eneo ndilo tunalolishia mifugo na ndilo linalotuwezesha kupata maziwa ya kulea watoto wetu. Tumehangaika kwa muda mrefu na sasa hatuna sehemu nyingine ya kuendeshea maisha yetu. Tumelala porini kwa siku kadhaa tukilinda mifugo huku wizi ukizidi. Tunakuomba usikie kilio chetu na utusaidie eneo letu lirudi kwa wananchi wa Alkaria.”

Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Mbunge wa Monduli, Isack Joseph, alisema maeneo ya malisho ni rasilimali ya wananchi na hayapaswi kumilikiwa na mtu binafsi kwa manufaa yake.

Alisema amesikitishwa na wingi wa malalamiko yanayomhusisha diwani huyo, akidai kuwa imekuwa kawaida kila anapoulizwa kuhusu tuhuma hizo kujibu kuwa ni siasa.

"Haiwezekani kila akituhumiwa jambo ajibu ni siasa. Kama wananchi wanaendelea kulalamika kwa uzito huu, lazima suala hili lichunguzwe. Nimekiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimuite ofisini ili ajibu tuhuma hizi na ukweli ujulikane," alisema Isack.

Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Sepeko, Kimai Diwani, alipoulizwa kuhusu madai hayo kwa njia ya simu, aliyakanusha vikali akisema ni sehemu ya kampeni za kumchafua kisiasa.

Alidai kuwa Mbunge wa Monduli amekuwa akiwashawishi baadhi ya wananchi kutoa malalamiko dhidi yake kutokana na tofauti za kisiasa zilizopo baina yao.

"Hakuna ukweli wowote katika tuhuma hizo. Haya ni maneno ya kisiasa yanayolenga kunichafua mbele ya wananchi. Mbunge anatakiwa ajikite katika kutekeleza majukumu yake badala ya kueneza chuki za kisiasa," alisema diwani huyo.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Wilaya ya Monduli, Waziri Juma, alisema Serikali tayari ilishaanza kushughulikia mgogoro huo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi.

Alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuitisha mkutano mkuu wa kijiji, kupima rasmi eneo la malisho, kuandaa hati ya eneo hilo na kuweka jumla ya bikoni 21 kwa ajili ya kuainisha mipaka yake.

Pamoja na hatua hizo, wananchi wa Alkaria walisema bado hawajaridhishwa kwani utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa haujakamilika, hivyo wameiomba Serikali kuharakisha mchakato huo ili eneo la malisho lirejeshwe rasmi kwa matumizi ya jamii na kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu.

Suala hilo linatajwa kuwa miongoni mwa migogoro ya ardhi inayozidi kuibua mvutano katika Wilaya ya Monduli, ambapo wananchi wanaitaka Serikali kuhakikisha sheria za ardhi zinasimamiwa kikamilifu na viongozi watakaobainika kukiuka taratibu wanachukuliwa hatua bila upendeleo.










Ends

Post a Comment

أحدث أقدم