TWARIQA YAMPA HESHIMA KUU RAIS SAMIA, YAMUALIKA DUA YA TAIFA ARUSHA,KUMWENZI HAYATI SALIMU DARUWEZI AGOST

TWARIQA YAMPA HESHIMA KUU RAIS SAMIA, YAMUALIKA DUA YA TAIFA

....Viongozi wa dini, vijana na wanawake wamemwomba aungane nao kuombea amani, umoja na maendeleo ya Tanzania

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

TAASISI ya Dini ya Kiislamu ya Twariqa imetoa mwaliko rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhudhuria Dua Kuu ya Taifa itakayofanyika Agosti 21 katika Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Zawia Kuu jijini Arusha.

Taasisi hiyo imesema ujio wa Rais Samia katika dua hiyo utakuwa ishara kubwa ya heshima, mshikamano na kutambua nafasi ya viongozi wa dini katika kuendeleza amani, upendo na umoja wa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Jumatano Julai,29,2026 Makao Makuu ya Twariqa, Zawia Kuu Arusha, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Haruna Hussein, alisema waumini wa Twariqa pamoja na Watanzania wengi wanamuomba Rais Samia kukubali mwaliko huo na kushiriki katika ibada maalumu ya kuliombea Taifa.

Alisema Dua Kuu hiyo itakuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa itaambatana na kumbukumbu maalumu ya kumuenzi mwasisi wa Taasisi ya Twariqa, Hayati Sheikh Salumu Daruweshi maarufu kwa jina la “Mti Mkavu”, ambaye alitoa mchango mkubwa katika kueneza mafundisho ya dini ya Kiislamu yenye misingi ya amani, upendo na mshikamano.

“Tunamualika kwa heshima kubwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria Dua Kuu ya Twariqa. Siku hiyo pia tutakuwa tunamuenzi mwasisi wetu Hayati Sheikh Salumu Daruweshi ‘Mti Mkavu’, ambaye aliacha alama kubwa katika historia ya taasisi hii na Taifa kwa ujumla,” alisema Sheikh Haruna.

Alisisitiza kuwa dua hiyo si tukio la kisiasa bali ni ibada maalumu yenye lengo la kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na maendeleo.

VIJANA TWARIQA: “AMANI NI URITHI WA TAIFA LETU”

Kwa upande wake, Kiongozi wa Vijana wa Taasisi ya Twariqa, Khalifa Juma, alisema vijana wana wajibu mkubwa wa kulinda amani ya nchi na kuhakikisha hawatumiki katika vitendo vinavyoweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa.

Alisema mwaliko wa Rais Samia katika dua hiyo unaonyesha heshima na kutambua mchango wa taasisi hiyo katika kujenga jamii yenye maadili mema.

“Tumekutana hapa kwa ajili ya maslahi ya taifa letu. Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja, mshikamano, kuheshimiana na kuvumiliana. Hizi ni tunu ambazo tunapaswa kuzilinda kwa nguvu zetu zote,” alisema Khalifa.

Aliwataka vijana kutumia nguvu zao, elimu na vipaji katika kujenga taifa badala ya kuruhusu kutumiwa kueneza chuki, vurugu au taarifa zisizo sahihi.

WANAWAKE TWARIQA: “MAMA YETU RAIS, KARIBU TUSHIRIKIANE KULIOMBEA TANZANIA”

Nao wanawake wa Taasisi ya Twariqa wametoa mwito kwa Rais Samia kuhudhuria dua hiyo maalumu, wakisema uwepo wake utaongeza nguvu ya umoja na mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake hao, Mariam Ali Mketo alisema:

“Mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sisi wanawake wa taasisi hii tunakukaribisha kwa moyo mmoja uje tushirikiane katika dua kubwa ya kuliombea Taifa letu la Tanzania.”

Alisema waumini wa Twariqa wanathamini uongozi wa Rais Samia na wanaendelea kumuombea hekima na afya njema katika kuliongoza Taifa.

Mketo pia alisisitiza umuhimu wa Watanzania kujenga maridhiano na umoja kabla ya masuala makubwa ya kitaifa, akisema masuala kama Katiba yanapaswa kuwa ajenda ya Watanzania wote bila kujikita katika misingi ya makundi.

“Hakuna Katiba ya chama, hakuna Katiba ya dini. Katiba ni ya Watanzania wote. Tunahitaji kukaa pamoja na kujenga maridhiano,” alisema.

MWENYEKITI TWARIQA: “TANZANIA HAITAKI VURUGU”

Mwenyekiti wa Taasisi ya Twariqa Twa Qadiria, Rehema Athmani, alisema wanawake wa Tanzania hawataki kuona taifa likiingia katika migogoro au vurugu kwa kuwa madhara makubwa huwapata zaidi wanawake na watoto.

Alisema amani ndiyo msingi wa maisha ya Watanzania na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda.

“Sisi kama wanawake hatuhitaji kabisa vurugu ndani ya Tanzania yetu. Tukitokea vurugu yoyote, wanaoumia zaidi ni wanawake na watoto. Tunachohitaji ni amani, upendo na kuishi kwa kuheshimiana,” alisema Rehema.

Amesema Tanzania imejijengea heshima kutokana na amani iliyopo na kuwataka wananchi kuendelea kuepuka kauli za chuki, matusi na uchochezi.

Aidha, alimkaribisha Rais Samia katika Dua Kuu ya Twariqa, akisema tukio hilo litakuwa nafasi ya kumuombea yeye na Taifa kwa ujumla.

“Karibu ndani ya Twariqa Twa Qadiria, taasisi iliyoasisiwa kwa misingi ya mafundisho ya Sheikh Salum Daruweshi (Mti Mkavu). Tutakuombea dua wewe na nchi yetu ili Tanzania iendelee kuwa na amani,” alisema.

Dua Kuu ya Twariqa inayotarajiwa kufanyika Agosti 21 jijini Arusha inatarajiwa kukutanisha waumini, viongozi wa dini na wageni mbalimbali kwa ajili ya kumuombea Rais, viongozi wa Taifa na amani ya Tanzania.





Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم