SERIKALI YAMPA HADHI MAALUM DEKKER, YAAHIDI KUONDOA VIKWAZO VYA UWEKEZAJI
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
SERIKALI imeitaja kampuni ya Maua ya Dekker Chrysanten Tanzania kuwa miongoni mwa wawekezaji wa kimkakati nchini, ikiahidi kuondoa changamoto zinazokwamisha shughuli zake ili kuongeza uzalishaji, ajira, mapato ya Serikali na fedha za kigeni.
Ahadi hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, Julai 25,2026 alipotembelea shamba la maua la kampuni hiyo lililopo Kijiji cha Maksoru, Kata ya Akeri, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambapo alisifu mchango wake mkubwa katika uchumi wa Taifa.
Dkt. Chaya alisema Dekker ni miongoni mwa kampuni zinazobeba uzito mkubwa katika sekta ya kilimo cha maua kutokana na kulipa zaidi ya Shilingi bilioni saba kwa mwaka kupitia kodi mbalimbali zikiwemo Corporate Tax, PAYE, Service Levy na tozo nyingine, sambamba na kuiingizia nchi fedha za kigeni kupitia mauzo ya maua katika masoko ya kimataifa.
Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wawekezaji wa aina hiyo wanapata mazingira bora ya kufanya biashara ili waendelee kupanua uwekezaji wao.
"Huyu ni mwekezaji wa kimkakati. Tunapaswa kumlea, kumlinda na kumwezesha azalishe zaidi kwa sababu mchango wake katika pato la Taifa, ajira na mapato ya Serikali ni mkubwa," alisema Dkt. Chaya.
Aliongeza kuwa mbali na kulipa kodi, Dekker imeendelea kutoa ajira kwa mamia ya Watanzania na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yake ya uwekezaji.
Naibu Waziri huyo alisema ziara za Serikali kwa wawekezaji zinalenga kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili zisiathiri uzalishaji.
Akizungumzia changamoto ya barabara inayoelekea shambani hapo, alisema Serikali itashirikiana na TAMISEMI, TARURA na wizara husika kuhakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na shughuli za uzalishaji.
Pia alisema Serikali imeanza maboresho ya mfumo wa marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kuondoa ucheleweshaji uliokuwa ukisababisha kampuni nyingi kukosa mtaji wa kuendesha shughuli zao.
"Tunataka wawekezaji wafanye kazi bila vikwazo. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wetu na ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya ajira na ukuaji wa uchumi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.
Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji kupitia sera zinazotabirika zinazovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
DEKKER YALILIA VAT YA SH. BILIONI 1.5
Katika ziara hiyo, uongozi wa Dekker uliiomba Serikali kuharakisha urejeshaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 za VAT, ukisema kuchelewa kwa fedha hizo kunakwamisha mtiririko wa fedha na kupunguza kasi ya utekelezaji wa miradi mipya ya uwekezaji.
Meneja wa shamba hilo, John Kivuyo, alisema pamoja na Tanzania kuwa na mazingira mazuri ya biashara, marejesho ya VAT kwa wakati ni muhimu kwa kampuni kuendelea kupanua uzalishaji.
"Kwa sasa tunaidai Serikali zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 za VAT. Fedha hizi ni sehemu ya mtaji wetu wa kuendesha shughuli za kila siku na kupanua uwekezaji," alisema.
Kivuyo alisema Dekker, kampuni yenye makao yake nchini Uholanzi, inaendesha mashamba matatu nchini ambayo ni Dekker Arusha, Dekker Kilimanjaro na Dekker Machame, huku ikiwa imeajiri zaidi ya wafanyakazi 1,360 moja kwa moja.
Alisema pamoja na kuwa miongoni mwa walipakodi wakubwa katika sekta ya maua, kampuni hiyo imeanza hatua mpya ya kupanua uwekezaji wake baada ya kununua shamba jipya katika eneo la Karangai, ambapo uzalishaji unatarajiwa kuanza mapema mwaka 2027.
"Tunaendelea kuwekeza kwa sababu tunaamini Tanzania ina mazingira mazuri ya biashara. Tunahitaji changamoto chache zilizobaki, ikiwemo marejesho ya VAT kwa wakati na kuboreshwa kwa miundombinu, zipatiwe ufumbuzi ili tuongeze uzalishaji, ajira na mapato ya Serikali," alisema Kivuyo.
Akijibu hoja hizo, Dkt. Chaya alisema Serikali itazifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na uongozi wa kampuni hiyo kwa kushirikiana na taasisi husika, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wawekezaji wanaendelea kufanya kazi katika mazingira yanayochochea ukuaji wa uchumi, uzalishaji na ajira.
Alisema Serikali itaendelea kutembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji nchini ili kusikiliza changamoto za wawekezaji na kuharakisha utatuzi wake kwa manufaa ya uchumi wa Taifa.
**ends**









Post a Comment