SERIKALI YAIPONGEZA A TO Z KWA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA DAWA CHA SH. BILIONI 20, YAHAIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU

SERIKALI YAIPONGEZA A TO Z KWA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA DAWA CHA SH. BILIONI 20, YAHAIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU

....Yasema mradi utaipunguzia Tanzania utegemezi wa vifaa tiba kutoka nje, kuongeza ajira na kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji Afrika Mashariki

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

SERIKALI imepongeza uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 20 uliofanywa na Kampuni ya A to Z Group katika ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha vifaa tiba kilichopo Kisongo, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ikisema ni hatua kubwa ya kuimarisha sekta ya afya, kukuza uchumi wa viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.



Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, alisema mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji wa kimkakati unaotekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda na uwekezaji wa ndani.

Alisema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza dawa na vifaa tiba kutoka nje, lakini sasa serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu.

"A to Z wameonyesha mfano wa uzalendo wa kweli kwa kuwekeza katika sekta nyeti ya afya. Huu ni uwekezaji utakaoongeza ajira, kuhamisha teknolojia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba katika ukanda wa Afrika Mashariki," alisema Dkt. Chaya.

Alibainisha kuwa serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Tano wa Taifa wa Maendeleo, ambao umeweka kipaumbele katika kuimarisha viwanda vya dawa na vifaa tiba kupitia sera rafiki za uwekezaji.

Naibu Waziri huyo alisema serikali imepokea changamoto zilizowasilishwa na uongozi wa kampuni hiyo, ikiwemo ubovu wa barabara inayoelekea kiwandani pamoja na hitaji la umeme wa uhakika, akiahidi kuwa zitatatuliwa kwa kuwa serikali imeweka fedha za kuboresha miundombinu katika maeneo ya uwekezaji.

"Tutahakikisha maeneo yote yenye uwekezaji mkubwa yanapata barabara bora, umeme wa uhakika na huduma nyingine muhimu ili viwanda viweze kuzalisha kwa ufanisi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa," alisisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa Masoko na Ushirikiano wa Kimataifa wa A to Z Group, Silvester Kazi, alisema kampuni hiyo imeamua kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 20 kujenga kiwanda hicho cha kisasa kwa lengo la kuongeza uwezo wa Tanzania kujitosheleza katika uzalishaji wa vifaa tiba vinavyotumika kila siku katika hospitali na vituo vya afya.

Alisema kiwanda hicho kitazalisha bidhaa muhimu zikiwemo sindano (syringes), vifaa vya kuongezea wagonjwa damu na maji mwilini (IV Sets) pamoja na vifaa vya kuongezea wagonjwa damu (Blood Transfusion Sets), ambavyo kwa sasa vinahitajika kwa wingi nchini na katika masoko ya kikanda.

"Teknolojia tuliyowekeza ni ya kisasa na inalenga kuzalisha vifaa tiba vinavyokidhi viwango vya kimataifa vya ubora. Uwekezaji huu utaongeza ajira, utaimarisha sekta ya afya na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa vifaa tiba katika ukanda huu," alisema Kazi.

Aliongeza kuwa A to Z Group imeendelea kuwa miongoni mwa wawekezaji wazalendo wakubwa nchini kwa kuajiri zaidi ya wafanyakazi 6,000, huku kiwanda hicho kipya kikitarajiwa kuongeza mamia ya nafasi nyingine za ajira na kuchochea ukuaji wa viwanda vinavyozalisha bidhaa za afya.

Ziara ya Dkt. Chaya katika kiwanda hicho imeonekana kuwa ishara ya dhamira ya serikali ya kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kimkakati vinavyochangia uhamishaji wa teknolojia.

Pia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuifanya Tanzania kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje, huku ikijijengea uwezo wa kuwa msambazaji mkuu wa dawa na vifaa tiba katika soko la Afrika Mashariki na Kati.










Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post