MAHAKAMA YA RUFANI YAMPA PIGO DPP KATIKA KESI YA TUNDU LISSU


MAHAKAMA YA RUFANI YAMPA PIGO DPP KATIKA KESI YA TUNDU LISSU

By Arushadigital|Dar Es Salaam

DAR ES SALAAM – Mahakama ya Rufani ya Tanzania leo, Julai 30, 2026, imetupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), yaliyokuwa yakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliokataa kuruhusu upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wa ziada katika kesi inayomkabili mwanasiasa Tundu Lissu.

Uamuzi huo unathibitisha msimamo wa Mahakama Kuu kwamba kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act - CPA) hakitoi mamlaka kwa upande wa mashtaka kumrejesha shahidi ambaye tayari alishamaliza kutoa ushahidi ili kuongeza ushahidi mwingine.

Asili ya mzozo huo ilianza Februari 18, 2026, pale Jamhuri ilipowasilisha Notisi ya Nyongeza ya Ushahidi (Notice of Additional Substance of Evidence), ikitaka kumwita tena shahidi wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amini Mahamba, kwa lengo la kuwasilisha ushahidi wa ziada.

Hata hivyo, Februari 24, 2026, Mahakama Kuu ilikataa ombi hilo baada ya kubaini kuwa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai hakiruhusu shahidi aliyeshatoa ushahidi kurejeshwa kwa ajili ya kuongeza ushahidi mwingine.

Kutokana na uamuzi huo, Machi 3, 2026, DPP aliwasilisha maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufani akidai kuwa Mahakama Kuu haikutafsiri ipasavyo masharti ya sheria husika. Maombi hayo yalisikilizwa Julai 3, 2026, kabla ya hukumu kutolewa leo.

Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja za Mahakama Kuu na kueleza kuwa tafsiri iliyotolewa kuhusu kifungu cha 308 ilikuwa sahihi kisheria. Mahakama ilisisitiza kuwa sheria hiyo haimpi upande wa mashtaka uwezo wa kumrudisha shahidi aliyeshatoa ushahidi ili kuongeza ushahidi mwingine.

Uamuzi huo unaonekana kuwa wa muhimu katika mfumo wa haki jinai nchini, kwani unaweka mwongozo wa kisheria kuhusu namna kifungu cha 308 kinavyopaswa kutafsiriwa na kutumika katika mwenendo wa kesi za jinai.

Aidha, hukumu hiyo inasisitiza umuhimu wa pande zote katika mashauri ya jinai kufuata taratibu zilizowekwa na sheria wakati wa kuwasilisha ushahidi, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kuzingatia misingi ya sheria na usawa wa kesi.

Ends...

Post a Comment

أحدث أقدم