LUKUMAY: SERA ZA SAMIA ZAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI ARUMERU,DKT CHAYA ATEMBELEA WAWEKEZAJI WAKUBWA WA MASHAMBA YA MAUA

 LUKUMAY: SERA ZA SAMIA ZAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI ARUMERU,DKT CHAYA ATEMBELEA WAWEKEZAJI WAKUBWA WA MASHAMBA YA MAUA

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

 

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan yameendelea kuvutia wawekezaji wakubwa nchini, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.


Akizungumza leo Julai 25,2026 wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, katika viwanda na miradi ya uwekezaji wilayani Arumeru, Lukumay alisema uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 20 uliofanywa na kampuni ya A to Z katika uzalishaji wa vifaa tiba ni ushahidi wa mafanikio ya sera hizo.


Alisema dhamira ya Serikali ni kuifanya Tanzania ijitegemee katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, hatua itakayoongeza ajira, kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kuongeza mauzo ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Akiizungumzia Kampuni ya Maua ya Dekker Chrysanten Tanzania, Lukumay alisema uwekezaji huo umeendelea kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika Wilaya ya Arumeru, ukiwa tayari umezalisha ajira kwa zaidi ya watu 1,300 huku maua yanayozalishwa yakisafirishwa katika masoko ya kimataifa na kuingiza fedha za kigeni nchini.

"Wawekezaji hawa si tu wanatoa ajira kwa wananchi wetu, bali pia wanaongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na kuiwezesha Tanzania kupata fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje," alisema.

Alibainisha kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa Tanzania kwa kuwa inaajiri takribani asilimia 70 ya Watanzania na kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya Serikali.

Lukumay alisema wananchi wa Arumeru Magharibi wanaendelea kumpongeza Rais Samia kwa kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji kupitia sera rafiki za biashara, diplomasia ya uchumi, utalii na utulivu wa kisiasa, mambo yaliyoongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Awali Naibu Waziri ofisi wa Nchi ofisi ya Rais (mipango na uwekezaji), dkt Pius Chaya alisema ziara za Serikali kwa wawekezaji zinalenga kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili zisiathiri uzalishaji.

Akizungumzia changamoto ya barabara inayoelekea katika maeneo ya uwekezani wa maua, alisema Serikali itashirikiana na TAMISEMI, TARURA na wizara husika kuhakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na shughuli za uzalishaji.

Pia alisema Serikali imeanza maboresho ya mfumo wa marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kuondoa ucheleweshaji uliokuwa ukisababisha kampuni nyingi kukosa mtaji wa kuendesha shughuli zao.

"Tunataka wawekezaji wafanye kazi bila vikwazo. Sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wetu na ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya ajira na ukuaji wa uchumi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji kupitia sera zinazotabirika zinazovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.


Ends..



Post a Comment

أحدث أقدم