KILIO CHA NDOO TUPU CHAZAA MATUNDA ,MABOMBA YA MAJI YA BILIONI 21 KUFIKA MONDULI JULAI 27, MBUNGE AWAHAKIKISHIA WANANCHI KUOGELEA MAJI KAMA MVUA!.

Na Joseph Ngilisho | MONDULI

KILIO cha muda mrefu cha wananchi wa Kata ya Naaalarami, Wilaya ya Monduli,Mkoani Arusha kuhusu ukosefu wa maji safi na salama, ambacho kilidhihirishwa kwa wanawake kubeba ndoo tupu wakati wa mapokezi ya Mbunge wa Monduli, Issac Joseph, sasa kimeanza kuzaa matunda baada ya mabomba ya mradi wa maji wa thamani ya Shilingi bilioni 21 kutarajiwa kuanza kupokelewa Julai 27 mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja baada ya wananchi kuwasilisha kwa vitendo changamoto ya maji inayowakabili, hali iliyosababisha hata zahanati mpya iliyokamilika katika kata hiyo kushindwa kuanza kutoa huduma kutokana na kukosekana kwa maji.

Wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Naaalarami, wanawake walifika wakiwa na ndoo tupu kama ishara ya mateso wanayopitia kila siku kutafuta maji. Tukio hilo liliibua hisia kubwa na kuwa ujumbe wa moja kwa moja kwa viongozi kuhusu umuhimu wa kutatua tatizo hilo.

Akizungumza katika mkutano huo, Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Kisongo, Paulina Richard, alisema ukosefu wa maji umeathiri kwa kiasi kikubwa huduma za afya, elimu na shughuli za maendeleo, huku wananchi wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji na kufuata huduma za matibabu.

Naye Mtendaji wa Kata ya Naaalarami, Fatina Yahaya, alisema changamoto hiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kata hiyo, akieleza kuwa zahanati iliyojengwa kwa gharama kubwa imeshindwa kuanza kutoa huduma kwa sababu ya ukosefu wa maji.

Akijibu malalamiko hayo, Mbunge wa Monduli, Issac Joseph, aliwahakikishia wananchi kuwa Kata ya Naaalarami itaunganishwa kwenye mradi mkubwa wa maji utakaohudumia vijiji 13 vya wilaya hiyo.

Mbunge huyo alisema atafuatilia utekelezaji wa mradi huo hadi mwisho na kusisitiza kuwa asingekuwa tayari kurudi kuomba kura kwa wananchi kama asingeweza kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika hatua ya kufuatilia utekelezaji wa mradi huo, Joseph ametembelea kiwanda cha kutengeneza mabomba jijini Dar es Salaam kujionea maendeleo ya utengenezaji wake, ambapo amesema mabomba hayo yako tayari kuanza kusafirishwa kuelekea eneo la mradi.

Alisema kuanzia Julai 27, mabomba hayo yataanza kupokelewa katika chanzo cha maji cha Ngaramtoni, Wilaya ya Arumeru, hatua inayoashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa sehemu muhimu ya mradi huo.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Monduli, Nelvin Msaki, amesema usafirishaji wa mabomba utafanyika kwa awamu kuanzia Julai 27, ambapo wastani wa kilomita 2.6 za mabomba utapelekwa kila siku ili kuharakisha ujenzi wa mradi huo.

Msaki alisema mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 21 ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa wilayani Monduli na unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji kwa maelfu ya wananchi waliokuwa wakikabiliwa na uhaba wa muda mrefu.

Mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 80,000 katika vijiji 13, huku ukitarajiwa kuondoa adha ya wanawake na watoto kutumia saa nyingi kutafuta maji na kuwezesha taasisi za afya na elimu kutoa huduma kwa ufanisi.

Kwa viongozi na wananchi wa Naaalarami, kuanza kuwasili kwa mabomba hayo ni ishara kwamba ujumbe walioutuma kupitia ndoo tupu umeanza kusikilizwa, na sasa wana matumaini ya kupata suluhisho la kudumu la tatizo la maji lililodumu kwa miaka mingi.


Ends..


Post a Comment

أحدث أقدم