MAKONDA AOMBA WADAU KUUNGANA KUFADHILI UPASUAJI WA WAGONJWA 258, AIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI

MAKONDA AOMBA WADAU KUUNGANA KUFADHILI UPASUAJI WA WAGONJWA 258, AIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, ameomba wadau, wafanyabiashara na watu wenye mapenzi mema kujitokeza kuunga mkono juhudi za kugharamia matibabu ya wagonjwa 258 waliobainika kuhitaji upasuaji baada ya uchunguzi uliofanyika katika kambi ya matibabu ya kibingwa iliyomalizika jijini Arusha.


Makonda ambaye pia ni waziri wa habari,utamaduni ,Sanaa na Michezo,akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa,alisema lengo ni kuhakikisha wagonjwa hao wanapata nafasi ya kufanyiwa upasuaji ili kurejesha matumaini, furaha na tabasamu kwa familia zao.

"Kwa upande wetu kama ofisi ya Mbunge na timu yetu, tunatamani kuwaona wagonjwa hawa wote 258 wanafika hatua ya pili ya kufanyiwa upasuaji. Tunaomba Mungu atufungulie milango na kuwagusa watu wenye uwezo na wenye huruma ili washiriki kuokoa maisha ya ndugu zetu," alisema Makonda.

Alisema kila mgonjwa atakayepata matibabu atakuwa ushuhuda wa thamani ya mshikamano wa jamii katika kuokoa maisha ya Watanzania.

Makonda aliongeza kuwa kama ilivyokuwa utamaduni wa kugusa maisha ya wananchi kupitia huduma mbalimbali, sasa ni wakati wa kuunganisha nguvu kuhakikisha wagonjwa hao wanapata matibabu yanayohitajika.

Aidha, alisema kambi hiyo imeacha mafanikio makubwa baada ya kubaki na dawa na vifaa tiba vyenye thamani kubwa ambavyo vitaendelea kutumika kuwahudumia wananchi wenye magonjwa mbalimbali katika vituo vya afya.

"Tulipata dawa nyingi kiasi kwamba zilibaki. Dawa hizo hazitapotea, zitaendelea kutumika kuwatibu wananchi wenye mahitaji mbalimbali ya kiafya. Huu ni ushahidi wa baraka ambazo Mungu ametujalia kupitia huduma hii," alisema.

Makonda pia alivipongeza vyombo vya habari kwa mchango mkubwa wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata huduma za afya kupitia taarifa na matangazo yaliyotolewa wakati wote wa kambi hiyo.

Alivitaja redio za Arusha pamoja na televisheni na vyombo vya habari vya kitaifa, ikiwemo BBC, kwa kazi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa wananchi hadi kuwafanya wengi waliokuwa wamekata tamaa kujitokeza kupata huduma.

Alisema ushirikiano wa wanahabari umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kambi hiyo na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uchunguzi na matibabu ya mapema.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم