WAGONJWA 258 KATI YA 20,871 WALIOHUDUMIWA KAMBI YA MAKONDA WAHITAJI RUFAA YA UPASUAJI BAADA YA KAMBI YA MATIBABU YA KIBINGWA ARUSHA

 WAGONJWA 258 WAHITAJI RUFAA YA UPASUAJI BAADA YA KAMBI YA MATIBABU YA KIBINGWA ARUSHA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amesema jumla ya wagonjwa 28,871 walihudumiwa katika kambi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi iliyofanyika jijini Arusha, huku wagonjwa 258 wakibainika kuhitaji rufaa kwa ajili ya upasuaji na matibabu ya kibingwa katika hospitali za rufaa.

Makonda alisema hayo leo Julai 23,2026 wakati akiongea na vyombo vya habari akisisitiza kuwa  huduma zilizotolewa zilihusisha magonjwa ya moyo, damu, watoto, wanawake na uzazi, upasuaji wa jumla, macho, mifupa, afya ya kinywa na meno, ngozi, figo na mfumo wa mkojo (Urology), masikio, pua na koo (ENT), tiba mazoezi, lishe, afya ya akili pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake.

Aidha, wananchi walipata elimu ya afya kuhusu kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ebola, kifua kikuu na Virusi vya UKIMWI, sambamba na huduma za dawa, maabara na uchangiaji damu.

Alisema huduma za ubingwa bobezi pia zilitolewa katika magonjwa ya moyo, mfumo wa fahamu (Neurosurgery), figo, mfumo wa mkojo na magonjwa ya damu.

Makonda alieleza kuwa mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa taasisi mbalimbali za afya nchini, zikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Kibong'oto, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Hospitali ya Selian pamoja na hospitali zote za halmashauri za Arusha, Arumeru, Monduli, Longido, Ngorongoro na Karatu.

Kwa mujibu wa Makonda, zaidi ya wataalamu wa afya 720, wakiwemo madaktari bingwa, wauguzi na watumishi wa kada mbalimbali, walishiriki kutoa huduma hizo, huku wastani wa wagonjwa 3,553 wakihudumiwa kwa siku, kiwango kilichovuka lengo la watu 2,000 kwa siku.

Alisema kati ya wagonjwa waliopata huduma, 258 walibainika kuhitaji upasuaji wa haraka na rufaa kwenda hospitali za juu, huku baadhi yao wakifanyiwa upasuaji papo hapo katika kambi hiyo kwa kutumia vyumba maalumu vya upasuaji vilivyowekwa kwenye magari ya kisasa.

Makonda alisema changamoto kubwa iliyobaki ni wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu yao baada ya kupatiwa rufaa.

Alitaja baadhi ya wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka kuwa ni mtoto wa mwaka mmoja kutoka Kisongo aliyebainika kuwa na tundu kwenye moyo linalohitaji matibabu yenye gharama ya takribani Sh milioni 27, mama mwenye saratani ya utumbo aliyeshindwa kufanyiwa upasuaji kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na ukosefu wa fedha, pamoja na mgonjwa mwingine aliyegundulika kuwa na uvimbe kwenye ubongo unaohitaji matibabu ya zaidi ya Sh milioni 15.

Makonda alisema serikali na wadau wanaendelea kutafuta utaratibu wa kuhakikisha wagonjwa hao wanapata matibabu ya kibingwa ili kuokoa maisha yao, akisisitiza kuwa lengo la kambi hiyo halikuwa kutoa dawa pekee bali kuhakikisha wagonjwa wanaohitaji matibabu ya juu wanafikishwa kwenye huduma stahiki.

ENDS 

Post a Comment

أحدث أقدم