BARABARA ZA AFCON 2027: MAKALLA ATOA ONYO KWA WALIOFIDIWA, TANROADS YAFICHUA MABADILIKO MAKUBWA ARUSHA
....Mhandisi Massawe: Mradi wa Sh bilioni 87.9 kuondoa mafuriko Majengo, Shamsi na Ngarenaro
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amewataka wananchi waliolipwa fidia katika maeneo yanayopitiwa na ujenzi wa barabara za maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kuondoka mara moja ili kutoa nafasi kwa wakandarasi kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo kwa kasi inayokusudiwa.
Agizo hilo limetolewa leo Julai 29, 2026, wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya barabara za kimkakati jijini Arusha, zinazotekelezwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya jiji kuelekea mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara za njia nne zenye urefu wa kilomita 9.1, kuanzia Makutano ya Ngarenaro hadi Mzunguko wa Kisongo, Makutano ya Ngarenaro hadi Kona ya Nairobi pamoja na Makutano ya Ngarenaro hadi Soko la Kilombero, huku Serikali ikitumia zaidi ya Sh bilioni 87.9 kugharamia utekelezaji wake.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, CPA Makalla alisema Serikali tayari imekamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa kwenye maeneo ya mradi, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa kazi hizo.
“Nimshukuru Rais kwa kuwezesha ujenzi wa barabara hizi. Serikali imeshalipa fidia wananchi wote wanaopitiwa na barabara za AFCON. Nawashukuru wale ambao tayari wameondoka kwa kuonesha uzalendo, lakini wale ambao bado hawajaondoka nawaomba waondoke ili kumpisha mkandarasi kuendelea na kazi,” amesema Makalla.
Amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa Jiji la Arusha, si tu katika maandalizi ya AFCON 2027, bali pia katika kupunguza msongamano wa magari, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na utalii.
TANROADS YAWEKA MKAKATI WA KUDHIBITI MAFURIKO
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amesema mradi huo umebeba suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya mafuriko ambayo yamekuwa yakilikabili baadhi ya maeneo ya jiji.
Mhandisi Massawe amesema pamoja na upanuzi wa barabara hizo kuwa njia nne, mradi huo unahusisha ujenzi wa mifumo mikubwa ya kupitisha maji, hatua ambayo itaondoa adha ya mafuriko katika maeneo ya Majengo, Shamsi na Ngarenaro.
Amesema miundombinu hiyo ya maji itajengwa kwa kuunganisha mifereji mikubwa itakayokusanya maji na kuyaelekeza katika Mto TANAPA, hivyo kupunguza athari zinazotokana na mvua kubwa.
“Mradi huu hauhusishi barabara pekee, bali pia umezingatia changamoto ya maji katika maeneo haya. Tutajenga mitaro mikubwa itakayosaidia kuondoa maji kwa ufanisi na kupunguza mafuriko ambayo yamekuwa tatizo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Massawe.
Aidha, amesema TANROADS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa na kwa muda uliopangwa, ili Arusha iwe tayari kupokea wageni na timu zitakazoshiriki AFCON 2027.
Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha miundombinu ya Jiji la Arusha ambalo linatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayohusika katika maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
Ends..




Post a Comment