CCM YAFANYA MABADILIKO MADOGO SEKRETARIETI, MWANRI ATEULIWA NAIBU KATIBU MKUU BARA
Na Joseph Ngilisho
ZANZIBAR – Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imefanya mabadiliko madogo ndani ya Sekretarieti ya chama hicho kwa kuwateua viongozi katika nafasi mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya chama.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Zanzibar, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema mabadiliko hayo yameidhinishwa na Kamati Kuu ili kuimarisha utendaji wa chama.
Katika uteuzi huo, Agrey Mwanri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na John Mongella, huku Abdi Mahmud Abdi akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.
Kihongosi alisema mabadiliko hayo pia yamegusa idara muhimu za chama ambapo Paul Chacha ameteuliwa kuwa Katibu wa NEC anayesimamia Idara ya Organizesheni, akichukua nafasi ya Issa Ussi Gavu.
Vilevile, Jamal Kassim ameteuliwa kuongoza Idara ya Uchumi, akirithi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Raila Burhan Ngonzi.
Pamoja na mabadiliko hayo, baadhi ya viongozi wameendelea kubaki katika nafasi zao, akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, Katibu wa NEC wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, pamoja na Katibu wa NEC wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid.
Mabadiliko hayo yanakuja wakati CCM ikiendelea kuimarisha safu yake ya uongozi kuelekea utekelezaji wa agenda mbalimbali za chama na maandalizi ya shughuli zake za kisiasa.
Ends..

Post a Comment