APSP YAPIGA HATUA, WATAALAMU WA UGAVI WAONYWA KULINDA HESHIMA YA TAALUMA
....Viongozi wa APSP wataka mageuzi ya ununuzi wa umma kupitia uadilifu, matumizi ya mifumo ya kidijitali na usimamizi madhubuti wa mikataba ili kuongeza thamani ya fedha za umma....
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
KAMISHNA wa zamani wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Frederick Mwakibinga, amesema taaluma ya ugavi na manunuzi nchini imeanza kuondokana na taswira ya kulaumiwa na sasa inaanza kutambuliwa kwa utendaji bora, huku akiwataka wataalamu kulinda uadilifu na weledi ili mafanikio hayo yasipotee.
Mwakibinga alitoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 28,2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Wanachama wa Chama cha Wataalamu wa Ugavi na Manunuzi Tanzania (APSP) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), akisema mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2020 yanaonesha sekta hiyo imeingia katika hatua mpya ya ukuaji.Alisema APSP imefanikiwa kuongeza idadi ya wanachama, kuimarisha mifumo ya uwajibikaji wa kifedha, kupata kiwanja cha makao makuu Dodoma, kusajili nembo ya chama, kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), pamoja na kushiriki kutafsiri mfumo wa kitaifa wa NeST kwa lugha ya Kiswahili.
"Mafanikio haya yanaonyesha kuwa APSP imevuka hatua ya kuanzishwa na sasa inajenga taasisi yenye misingi imara, mifumo madhubuti na matokeo yanayoonekana. Hii ni kazi kubwa inayostahili pongezi," alisema.
Katika kauli iliyobeba uzito wa mabadiliko ya taswira ya taaluma hiyo, Mwakibinga ambaye pia ni mlezi wa APSP alisema miaka ya nyuma wataalamu wa ugavi walihusishwa zaidi na lawama, lakini hali hiyo imeanza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa watumishi wanaotambuliwa kwa utendaji bora katika taasisi mbalimbali za umma.
Aidha alisisitiza kwa kutoa rai kwa wataalamu wa ugavi na manunuzi kusimamia vema taaluma yao kwa kulinda mikataba inayoingiwa na taasisi mbalimbali ili kuepusha upotevu wa fedha za Umma.
"Kwa muda mrefu taaluma yetu ilikuwa ikihusishwa na lawama, lakini leo tunaanza kushuhudia wataalamu wa ugavi wakisifiwa na kutambuliwa kwa utendaji bora. Hii ni hatua kubwa ambayo hatupaswi kurudi nyuma," alisema.
Alionya kuwa mafanikio hayo yataendelea kudumu iwapo wataalamu wataendelea kuzingatia uadilifu, weledi na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao.
"Mtu anayefanya kazi kwa weledi ni rahisi kutetewa na kupewa nafasi za maendeleo. Lakini ukiingia katika vitendo vinavyoharibu taaluma, hata wanaotaka kukusaidia hushindwa kufanya hivyo," alisisitiza.
Mwakibinga pia aliwataka wanachama kushiriki kikamilifu katika tafiti, makongamano ya kitaaluma na mijadala ya kitaifa na kimataifa ili kuongeza ushindani wa taaluma ya ugavi na manunuzi, huku akiwapongeza wataalamu walioshiriki kutafsiri mfumo wa NeST kwa Kiswahili akisema hatua hiyo imeongeza thamani ya sekta ya ununuzi wa umma nchini.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa APSP, Dkt. Emmanuel Urembo, alitoa wito wa mageuzi makubwa katika mfumo wa ununuzi wa umma kwa kuwataka wataalamu kuimarisha mipango ya ununuzi, matumizi ya teknolojia za kidijitali na usimamizi wa mikataba ili kuongeza thamani ya fedha za umma na kuziba mianya ya ubadhirifu.
Dkt. Urembo alisema mafanikio ya taasisi nyingi za umma yanategemea ubora wa mipango ya ununuzi na bajeti, akieleza kuwa maandalizi yanayofanyika kwa wakati huokoa fedha, muda na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kuzingatia misingi minne ya Value for Money ambayo ni uchumi, ufanisi, matokeo na usawa, akisema hiyo ndiyo dira ya ununuzi wa kisasa duniani.
Aidha, alionya dhidi ya vitendo vinavyoharibu ushindani wa haki katika zabuni, ikiwemo mzabuni mmoja kutumia kampuni nyingi kushindania zabuni moja, huku akihimiza matumizi makubwa ya mfumo wa NeST na mifumo mingine ya kidijitali ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kasi ya utoaji wa huduma.
Dkt. Urembo alisema changamoto kubwa haipo katika utoaji wa zabuni pekee bali katika usimamizi wa mikataba, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa, kazi na huduma zinazopokelewa zinaendana na masharti yaliyokubaliwa.
Pia aliwataka wataalamu kuhakikisha taasisi zao zinazingatia maelekezo ya Serikali ya kutenga angalau asilimia 30 ya thamani ya ununuzi kwa makundi maalumu na kutumia mifumo ya ufuatiliaji ya PPRA kubaini mapema vihatarishi vya ukiukwaji wa sheria za ununuzi.
Kauli za viongozi hao zinakuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika ununuzi wa umma kama sehemu ya kuongeza uwazi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha kila fedha ya umma inaleta thamani inayokusudiwa kwa wananchi.



إرسال تعليق