ALIYEWAUA BABA YAKE MZAZI NA BABA MDOGO NA KUWAFUKIA NYUMBANI DAR AKAMATWA

 ALIYEWAUA  BABA YAKE MZAZI NA BABA MDOGO NA KUWAFUKIA NYUMBANI DAR AKAMATWA

Na Arushadigital| DAR ES SALAAM

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linamshikilia kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Hosamu Hamza maarufu Maopena, kwa tuhuma za kuwaua baba yake mzazi pamoja na baba yake mdogo kwa kutumia shoka na kisha kuwafukia ndani ya eneo la nyumba yao iliyopo Mtaa wa Sindano, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026 majira ya saa 9 alasiri katika eneo la Makongo akiwa na kisu kilichokuwa na damu pamoja na mavazi yaliyokuwa yamechafuliwa na damu. Baada ya kukamatwa, alipelekwa katika kituo cha Polisi kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi zaidi.

Polisi wamesema baadaye usiku walipokea taarifa kutoka kwa wananchi waliokuwa na wasiwasi baada ya watu watatu waliokuwa wanaishi katika nyumba moja Mtaa wa Sindano kutokuwa wameonekana kwa muda, huku ndani ya nyumba hiyo kukiwa na damu nyingi iliyozua hofu.

Kutokana na taarifa hiyo, maofisa wa Polisi waliinza uchunguzi wa kina kwa kutumia mbinu za kisayansi na kubaini kuwa watu wawili walikuwa wameuawa na kufukiwa ndani ya shimo lililokuwa katika eneo la nyumba hiyo.

Miili iliyopatikana ilitambulika kuwa ni ya Hamza Juma Omari (Mautila) mwenye umri wa miaka 48 pamoja na Ally Juma Omari, mwenye umri wa miaka 37.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa, Hosamu Hamza Juma maarufu Maopena, ambaye ni mtoto wa marehemu Hamza Juma Omari, ndiye anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo dhidi ya baba yake mzazi na baba yake mdogo kabla ya kuwafukia katika eneo la makazi yao.

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi kuhusu chanzo na sababu za tukio hilo unaendelea, huku likiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kubaini ukweli wa tukio hilo na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika.

Polisi wameeleza kuwa mtuhumiwa ataendelea kushikiliwa wakati uchunguzi ukikamilishwa kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Post a Comment

Previous Post Next Post