LUKUMAY AWAHAKIKISHIA WANANCHI WA LENGIJAVE, ASISITIZA USHIRIKIANO NA KUSIKILIZA KERO
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameendelea na ziara yake ya siku ya tatu ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Lengijave, ambapo alijitambulisha rasmi kwa wananchi, kuwashukuru kwa imani waliompa katika uchaguzi mkuu na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, Dkt. Lukumay alisema amefika Lengijave kutimiza ahadi yake ya kukutana ana kwa ana na wananchi, kujionea maendeleo yanayotekelezwa na kupata nafasi ya kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali.
Aliwashukuru wananchi wa Lengijave kwa kumpa kura nyingi zilizomwezesha kuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, pamoja na kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi, akisema imani hiyo ni deni ambalo atalilipa kwa kuwatumikia kwa uadilifu na kuhakikisha maendeleo yanafika kwa kila mwananchi.
"Nimekuja kuwashukuru kwa imani kubwa mliyonipa. Kura zenu siyo za bure, ni dhamana ambayo itanifanya niendelee kuwatumikia kwa nguvu zangu zote. Mimi ni mbunge wa wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa, na lengo letu sasa ni maendeleo," alisema Dkt. Lukumay.
Mbunge huyo alimpongeza Diwani wa Kata ya Lengijave kwa ushirikiano anaouonyesha katika kusukuma maendeleo ya wananchi, akisisitiza kuwa baada ya uchaguzi hakuna sababu ya kuendeleza migawanyiko ya kisiasa bali kila kiongozi anapaswa kushirikiana kwa maslahi ya wananchi.
Katika mkutano huo, Dkt. Lukumay alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo, ikiwemo mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa Lengijave ambao unalenga kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Aidha, alisema Serikali itaendelea kuboresha huduma za elimu kwa kushughulikia changamoto zilizopo katika shule za kata hiyo kupitia ushirikiano wa wataalamu wa halmashauri na wadau wa maendeleo.
Mbunge huyo aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akieleza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika sehemu ya kusikiliza wananchi, wakazi wa Lengijave waliwasilisha kero mbalimbali zikiwemo changamoto za maji, miundombinu ya barabara, elimu, huduma za afya na masuala ya kilimo, huku Dkt. Lukumay akiwaahidi kuzifuatilia kwa karibu na kuzifikisha kwenye mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.
Alisisitiza kuwa ofisi yake itaendelea kuwa wazi kwa wananchi wote na kwamba ataendelea kufanya ziara za mara kwa mara katika kata zote za jimbo hilo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ubora na changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Ends .








Post a Comment