WATUHUMIWA WANNE WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA RAIA WA CHINA DAR ES SALAAM
Na Arushadigital | Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya raia wa China, Mr. Ge Baozhung, yaliyotikisa jiji la Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao walipanga njama za kumuibia marehemu kabla ya kutekeleza shambulio hilo usiku. Watuhumiwa hao wanadaiwa kuvamia eneo alilokuwapo marehemu, kumuibia kiasi cha shilingi milioni tisa na kisha kumuua ili kuficha ushahidi wa uhalifu wao.
Polisi wameeleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa ndani ya kiwanda kinachomilikiwa na marehemu. Baada ya kutekeleza uhalifu huo, watuhumiwa walikimbia na kuelekea maeneo mbalimbali nchini ambapo walitumia sehemu ya fedha walizoiba kununua ng’ombe na kufanya matumizi mengine binafsi.
Katika operesheni maalumu ya ufuatiliaji na uchunguzi, watuhumiwa wawili walinaswa katika eneo la Namanga mkoani Arusha wakati wakijaribu kujificha, huku wengine wawili wakikamatwa katika eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam katika nyakati tofauti.
Jeshi la Polisi limesema kuwa baada ya mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika kupanga na kutekeleza tukio hilo la ujambazi na mauaji. Aidha, uchunguzi unaendelea ili kubaini kama kuna watu wengine waliohusika katika mtandao huo wa uhalifu.
Polisi wamewahakikishia wananchi kuwa hatua zote za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao na kwamba watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi ili kujibu mashitaka yanayowakabili.
Jeshi hilo limeendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati, hatua ambayo imekuwa muhimu katika kufanikisha ukamataji wa wahalifu na kudumisha amani na usalama nchini.
Ends..
