TANZANIA YAONGEZA KASI KUFIKIA ASILIMI 80 YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKI IFIKAPO 2034

 MAKAMBA: TANZANIA YAONGEZA KASI KUFIKIA ASILIMIA 80 YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA IFIKAPO 2034

Na Joseph Ngilisho | Arusha

 

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, huku kiwango cha matumizi ya nishati hiyo kikiongezeka kwa kasi kutokana na juhudi za Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Makamba alisema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa nishati safi ya kupikia, ambapo aliwapongeza waandaaji wa mkutano huo wakiwemo Wizara ya Nishati, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na wadau wengine kwa mchango wao katika kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.

Alisema kaulimbiu ya mkutano huo, “Advancing Tanzania’s Clean Cooking Future: Progress, Partnerships and Pathways Towards 80% Accessibility by 2034,” inaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika.

“Kaulimbiu hii inaendana moja kwa moja na azma ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata nishati safi, salama, nafuu na endelevu ya kupikia. Hii ni ajenda ya kitaifa yenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Makamba.

Alieleza kuwa mkutano huo umejikita katika kujadili mafanikio na mafunzo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, mahitaji ya kifedha ya kuhamia katika matumizi ya nishati hiyo, biashara ya kaboni, sera na kanuni, mabadiliko ya tabianchi, ushirikishwaji wa wadau pamoja na mifumo ya uratibu na ufuatiliaji wa takwimu.

Makamba alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni suala linalogusa sekta nyingi kwa wakati mmoja, ikiwemo afya, mazingira, uchumi wa kaya, usawa wa kijinsia, elimu, uwekezaji na ajira.

Alibainisha kuwa matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu yamekuwa yakichangia magonjwa yanayotokana na moshi wa majumbani, hasa kwa wanawake na watoto, huku pia yakisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kuongeza gharama za kijamii na kiuchumi.

“Ndiyo maana Serikali imeifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa moja ya vipaumbele vyake. Kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, tumedhamiria kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imeanza kuona matokeo chanya ya juhudi hizo ambapo kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia kimeongezeka kutoka asilimia 6.6 mwaka 2021 hadi kufikia zaidi ya asilimia 28.6 katika miaka ya karibuni.

Kwa mujibu wa Makamba, mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa usambazaji wa gesi ya kupikia (LPG), ongezeko la matumizi ya majiko ya umeme, kampeni za uhamasishaji wa jamii, ushiriki wa sekta binafsi pamoja na maboresho ya sera yanayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Aidha, alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kupitia sera, mikakati na miongozo mbalimbali, hatua iliyowezesha utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa mitungi ya gesi, matumizi ya biogesi katika taasisi na kuhamasisha matumizi ya umeme kwa shughuli za kupikia.

Akizungumzia mafanikio ya mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Makamba alisema zaidi ya dola za Marekani milioni 10.1 sawa na takribani Sh bilioni 26.5 zimetolewa kama ruzuku kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati zaidi ya 100 wanaojihusisha na biashara ya nishati safi ya kupikia.

Alisema kupitia mradi huo, zaidi ya kaya 620,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza na maeneo mengine zimeanza kunufaika na teknolojia za nishati safi ya kupikia.

Vilevile, taasisi mbalimbali zimewezeshwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua iliyowanufaisha zaidi ya wanafunzi 62,000 nchini.

Katika hatua nyingine, Makamba alisema Serikali imepokea kifaa maalumu cha kisasa cha kupima ubora wa nishati safi ya kupikia (Emission Analyzer) kitakachosaidia kuthibitisha viwango vya ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini au kuagizwa kutoka nje.

Aliitaka Tume ya Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kusimamia ubora wa bidhaa hizo ili kuhakikisha usalama wa watumiaji na kuimarisha imani ya wananchi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mwisho, Makamba aliwashukuru Umoja wa Ulaya na UNCDF kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia nchini na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wanaounga mkono juhudi hizo.

“Milango yetu iko wazi wakati wote. Tutaendelea kushirikiana na wadau wote wanaotaka kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake ya nishati safi ya kupikia chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa ajenda hii barani Afrika,” alisema Makamba.




Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post