WATOTO WATATU WA FAMILIA MOJA WAUAWA KIKATILI , MIILI YAPATIKANA IKIWA HAINA BAADHI YA VIUNGO

 WATOTO WATATU WA FAMILIA MOJA WAUAWA KIKATILI LINDI, MIILI YAPATIKANA IKIWA HAINA BAADHI YA VIUNGO

Na Arushadigital |RUANGWA

Taharuki na simanzi vimetanda katika Kijiji cha Kilimahewa, Kata ya Nachingwea, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, kufuatia tukio la kusikitisha la kuuawa kwa watoto watatu wa familia moja ambao miili yao ilikutwa ikiwa haina baadhi ya viungo vya mwili.

Watoto hao, wenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka sita na saba, wanadaiwa kupotea tangu Juni 8, 2026 majira ya saa moja asubuhi walipokuwa wakielekea madrasa kama ilivyokuwa kawaida yao.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, baada ya kutoweka kwa watoto hao, familia kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ilianza jitihada za kuwatafuta katika maeneo mbalimbali bila mafanikio.

Hata hivyo, juhudi hizo zilichukua sura mpya ya majonzi baada ya miili ya watoto wawili kupatikana Juni 13, 2026 ikiwa imetelekezwa kichakani katika mazingira ya kutatanisha. Siku iliyofuata, Juni 14, mwili wa mtoto wa tatu ulipatikana katika eneo hilo hilo, na hivyo kuthibitisha vifo vya watoto wote watatu.

Taarifa zinaeleza kuwa watoto hao waliuawa kwa kunyongwa kabla ya miili yao kutupwa, huku ikibainika kuwa baadhi ya viungo vya miili yao vilikuwa vimeondolewa, jambo ambalo limeongeza hofu na maswali mengi miongoni mwa wananchi wa eneo hilo.

Kufuatia tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Lindi ilifika nyumbani kwa familia iliyopoteza watoto hao kwa ajili ya kutoa pole na kuwafariji ndugu pamoja na wananchi walioguswa na tukio hilo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP John Imori, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu huku vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa mauaji hayo.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni maalumu ya kuwatafuta watuhumiwa waliohusika na tukio hilo, huku akisisitiza ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili. Tunawaomba wananchi watulie na waendelee kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahusika wa uhalifu huu wa kinyama,” amesema ACP Imori.

Tukio hilo limeibua huzuni kubwa miongoni mwa wakazi wa Ruangwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla, huku wananchi wakitaka hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo ya kikatili.


Enda

Post a Comment

Previous Post Next Post