WATATU WANASWA WAKIJARIBU KUTOROSHA MIFUGO 852 KWENDA NCHI JIRANI

WATATU WANASWA WAKIJARIBU KUTOROSHA MIFUGO 852 KWENDA NCHI JIRANI

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA 

Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa wakijaribu kutorosha mifugo 852, ikiwemo ng'ombe, mbuzi na kondoo, kwenda nchi jirani kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, amesema operesheni hiyo ilifanyika wakati wa doria ya pamoja iliyotekelezwa katika Kijiji cha Matelea, Kata ya Matelea, Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika harakati za kusafirisha mifugo hiyo bila kufuata taratibu na sheria zinazosimamia usafirishaji wa mifugo kuvuka mipaka ya nchi, jambo ambalo linaikosesha Serikali mapato na kuhatarisha usalama wa sekta ya mifugo.

"Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalumu katika maeneo ya mipakani ili kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa mifugo na uhalifu mwingine unaohusiana na sekta hii muhimu ya uchumi," amesema Kamanda Pasua.

Ameeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini mtandao mzima uliokuwa ukihusika na jaribio hilo la utoroshaji, huku taratibu za kisheria dhidi ya watuhumiwa hao zikiendelea.

Kamanda Pasua pia amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote wanaposafirisha mifugo ndani na nje ya nchi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, akisisitiza kuwa utoroshaji wa mifugo si tu kwamba unaikosesha Serikali mapato, bali pia huchochea kuenea kwa magonjwa ya mifugo, kuhatarisha afya ya mifugo na kukiuka misingi ya ustawi na haki za wanyama.

..Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post