TWARIQA YAMTEUA MARIAM ALLY MKETO KUONGOZA IDARA YA MAMBO YA NJE, YAMWALIKA RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
TAASISI ya dini ya Twariqa Qadiria Jailania Arrasziqia Tanzania imemteua , Mariam Ally Mketo kuwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Idara ya Mambo ya Nje, huku ikitangaza maandalizi ya shughuli kubwa za kidini na kijamii zitakazofanyika mwezi Agosti mwaka huu na kumwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza katika kikao maalumu cha viongozi na wajumbe wa taasisi hiyo, Katibu Mkuu wa Twariqa Tanzania, Sheikh Haruna Hussein, alisema uteuzi wa Bi. Mariam umefanyika kwa mujibu wa katiba ya taasisi na unalenga kuimarisha utendaji kazi wa idara inayosimamia mahusiano na ushirikiano wa taasisi hiyo ndani na nje ya nchi.
Alisema uongozi una imani kubwa kuwa Mariam Ally Mketo atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kusaidia kuimarisha ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii, hususan wanawake na vijana katika shughuli za taasisi hiyo.
Katika hatua nyingine, Sheikh Haruna alitangaza kuundwa kwa Bodi ya Habari ya Idara ya Mambo ya Nje ambayo itakuwa na jukumu la kuratibu mawasiliano na kuhakikisha taarifa za taasisi zinawafikia wanachama na umma kwa wakati.
Katibu Mkuu huyo alisema kamati maalumu tayari imeanza maandalizi ya shughuli kubwa zinazotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, zikiwemo ibada maalumu, mikutano ya kidini, kampeni za upandaji miti na uchangiaji damu, ambazo zinalenga kuunga mkono juhudi za maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira pamoja na kumbukumbu ya kifo cha Kiongozi wa Taasisi hiyo Salimu Daruweshi Maarufu 'Mti Mkavu'.
Alisema taasisi hiyo imeanza mchakato wa kuwafikia wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa mafanikio makubwa.
“Tunatarajia kuwa na mkusanyiko mkubwa wa waumini kutoka Tanzania na nchi jirani. Maandalizi yanaendelea vizuri na tunawaomba wadau wote kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha shughuli hizi muhimu,” alisema.
Sheikh Haruna alibainisha kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika tarehe 21 Agosti katika eneo la Vyuo Vikuu, ambapo taasisi hiyo imemwalika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo muhimu.
Alisema uwepo wa Rais Samia utakuwa ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya taasisi za dini na Serikali katika kukuza amani, umoja na maendeleo ya taifa.
“Tumemualika Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu ya mwezi Agosti. Tunaamini uwepo wake utatoa hamasa kubwa kwa waumini na wananchi kwa ujumla katika kuendeleza ajenda za amani, mshikamano na maendeleo,” alisema.
Aidha, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanawezekana pale ambapo wananchi wanaishi kwa umoja na kuheshimiana.
Alimalizia kwa kuwapongeza wajumbe wa kamati za maandalizi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji na weledi ili kuhakikisha shughuli za mwezi Agosti zinakuwa za mafanikio makubwa kwa taasisi hiyo na taifa kwa ujumla.
**Ends***







