WANAWAKE WAHIMIZWA KUSHIKA USUKANI MAPINDUZI YA KIDIJITALI AFRIKA MASHARIKI

 WANAWAKE WAHIMIZWA KUSHIKA USUKANI MAPINDUZI YA KIDIJITALI AFRIKA MASHARIKI

Na Joseph Ngilisho |Arusha

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rebecca Kadaga, ametoa wito kwa wanawake wa ukanda wa Afrika Mashariki kuongeza ushiriki wao katika mapinduzi ya teknolojia ya kidijitali, akisisitiza kuwa maendeleo ya sasa ya kiteknolojia yanapaswa kuwa jumuishi na kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.

Kadaga alitoa wito huo jijini Arusha wakati wa Kongamano la Pili la Majadiliano ya Wanawake Kizazi kwa Kizazi la Afrika Mashariki (EAC), ambalo limewakutanisha wanawake viongozi, wataalamu na vijana kutoka nchi wanachama wa EAC kujadili nafasi ya mwanamke katika uongozi wa kidijitali na mageuzi ya kiuchumi yanayoendeshwa na teknolojia.

Amesema kuwa dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia kama akili bandia (AI), mifumo ya kifedha ya kidijitali (fintech), majukwaa ya biashara mtandaoni na ubunifu wa kidijitali, hivyo wanawake hawana budi kuingia kwa nguvu katika sekta hizo ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.

Kadaga alibainisha kuwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia hautazaa matunda iwapo hakutakuwa na uwekezaji katika elimu ya kidijitali, mafunzo ya stadi za kisasa na mazingira rafiki ya biashara yanayowezesha wanawake kushindana kwa usawa na makundi mengine.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Stephen Mbundi, amesema EAC inaendelea kuimarisha sera na mikakati inayolenga kuhakikisha usawa wa kijinsia unajikita katika ajenda ya mageuzi ya kidijitali ndani ya ukanda huo.

Amesema ongezeko la matumizi ya intaneti, huduma za kifedha mtandaoni na mifumo ya kidijitali ya biashara linahitaji ushiriki mpana wa wanawake na vijana ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa kikanda unakuwa shirikishi na wenye manufaa kwa wananchi wote.

Mbundi aliongeza kuwa jumuiya hiyo inaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuboresha miundombinu ya TEHAMA, pamoja na kuweka mazingira yatakayowezesha ubunifu na uwekezaji unaoendeshwa na teknolojia.

Mwakilishi wa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, George Odongo, amesema mabunge ya kikanda kwa kushirikiana na taasisi nyingine za EAC yanaendelea kuimarisha uandaaji na upitishaji wa sheria zinazohusu usawa wa kijinsia, ulinzi wa watumiaji wa mifumo ya kidijitali na maendeleo ya TEHAMA.

Amesema ushirikiano kati ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA), serikali za nchi wanachama na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha wanawake na vijana wanakuwa sehemu ya maamuzi katika sekta ya teknolojia badala ya kubaki kama watumiaji pekee.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake wa EALA, Fatuma Ndangiza, amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu kati ya viongozi waandamizi na kizazi kipya cha wanawake wenye ubunifu katika nyanja za kidijitali.

Ndangiza alieleza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi ya uongozi katika mapinduzi ya kidijitali, huku akisisitiza umuhimu wa elimu, ushirikishwaji wa kijamii na ulinzi wa wanawake dhidi ya changamoto za kimtandao kama unyanyasaji na ubaguzi.

Hitimisho la Mkutano

Kongamano hilo limehitimishwa kwa wito wa pamoja kutoka kwa washiriki wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwekezaji katika elimu ya TEHAMA, kuboresha usalama mtandaoni na kuhakikisha upatikanaji sawa wa fursa za kidijitali kwa wanawake na wasichana katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Washiriki wamesema mustakabali wa uchumi wa kikanda unategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea duniani.



Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post