WANANCHI 474 PANGANI KUANZA KULIPWA FIDIA KUPISHA MRADI WA MIWA NA KIWANDA CHA SUKARI WA DOLA MILIONI 350
Na Hadija Bagasha | Tanga
Wananchi 474 wa Vijiji vya Mseko na Kigurusimba katika Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga, wameanza kunufaika na malipo ya fidia ili kupisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 350, unaotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi katika eneo hilo na nchini kwa ujumla.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, kupunguza utegemezi wa uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi, kuimarisha ajira na kukuza shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Tanga.
Akizindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wanaostahili, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema hatua hiyo inaashiria mwanzo wa utekelezaji wa mradi ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Pangani pamoja na wadau wa maendeleo.
Alieleza kuwa eneo la hekta 22,000 limetengwa kwa ajili ya uwekezaji huo na kwamba baada ya kukamilika kwa tathmini ya ardhi pamoja na mali za wananchi, serikali kupitia TISEZA imeanza rasmi kulipa fidia kwa wananchi wote waliothibitishwa kustahili.
“Zoezi hili limeanza kwa wananchi ambao tayari wamekamilisha taratibu zote zinazohitajika. Serikali itaendelea kuwapa nafasi wale ambao bado hawajakamilisha nyaraka zao ili nao waweze kupata haki zao kwa wakati,” alisema Dkt. Burian.
Aliongeza kuwa zaidi ya wananchi 400 tayari wamesaini nyaraka muhimu za malipo, hatua inayowezesha mchakato huo kuendelea kwa haraka huku serikali ikihakikisha haki za wananchi wote zinalindwa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na taasisi zinazotekeleza mradi huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu na maslahi ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa taasisi hiyo, Remigius Reverius Ruttasitara, alisema wananchi wote 474 waliothibitishwa kulipwa fidia wanatarajiwa kukamilishiwa malipo yao kabla ya Juni 30, 2026.
Alisema kukamilika kwa zoezi hilo kutafungua rasmi hatua ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao unatarajiwa kuleta manufaa makubwa katika sekta za kilimo, viwanda, biashara na ajira.
“Tunaendelea kuwasisitiza wananchi wote wanaohusika kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zote zinazohitajika ili kurahisisha mchakato wa malipo na kuepusha ucheleweshaji usio wa lazima,” alisema Ruttasitara.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masaika, George Tadeo Mariano, alisema wananchi wa eneo hilo wameupokea mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na matarajio ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuzalisha maelfu ya nafasi za ajira kwa vijana, kukuza biashara ndogo na za kati pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za kijamii na shughuli nyingine za maendeleo katika vijiji vinavyouzunguka.
Baadhi ya wananchi wa Vijiji vya Mseko na Kigurusimba walieleza matumaini yao kuwa uwekezaji huo utakuwa kichocheo cha maendeleo mapya katika Wilaya ya Pangani, huku wakiiomba serikali na wawekezaji kuhakikisha utekelezaji wake unaendelea kwa uwazi, ushirikishwaji na kuzingatia maslahi ya wananchi katika kila hatua.
Mradi wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari unatarajiwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi katika Mkoa wa Tanga, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, kuimarisha usalama wa chakula na malighafi za viwandani, kuongeza mapato ya serikali na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa kukamilika kwa zoezi la fidia, Pangani sasa inaingia katika hatua mpya ya maendeleo ya viwanda na kilimo cha kisasa, huku matarajio makubwa yakielekezwa kwenye ajira, biashara na ustawi wa wananchi wa eneo hilo.
Ends




Post a Comment